Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John (katikati), akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake na Kodi
...........................................
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Tanga imewataka wanawake wajasiriamali kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa jukwaa la “Wanawake na Kodi” mjini Tanga.
Akizungumza katika jukwaa hilo, John alisema lengo ni kuwawezesha wajasiriamali wanawake kupata elimu ya kodi kwa njia rahisi na kujiunga rasmi na mifumo ya kodi.
“Jukwaa hili ni daraja kati ya TRA na wajasiriamali wanawake. Tunataka waweze kulipa kodi kwa wakati na kuepuka biashara za siri,” alisema.
Alionya dhidi ya biashara zinazotumia njia za panya, akisema zinaihosha serikali mapato. Pia aliwataka wafanyabiashara kudai stakabadhi kila wanaponunua bidhaa.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania [JWT], Ismail Masudi, alisema ukwepaji kodi ni tabia mbovu inayodhoofisha uchumi.
“Wengi wakilipa kodi, itakuwa rahisi kuwabaini wale wasiolipa. Wanawake wajasiriamali wanapaswa kuongoza mabadiliko haya,” alisema Masudi.
Kaimu Meneja wa Elimu kwa Walipa Kodi, Charles Mkumbwa, alisema jukwaa hilo ni hatua ya kimkakati ya kuwafikia wanawake wajasiriamali ili kuimarisha ushiriki wao kiuchumi.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tanga, Charles Mtali, alibainisha kuwa wanawake wanachangia takriban asilimia 80 ya nguvu kazi na wanamiliki asilimia 54 ya biashara za kati na ndogo nchini.
Baadhi ya washiriki katika jukwaa hilo walisema wanashukuru TRA kwa kufanya utaratibu kuwapa elimu lakini pia wameenda mbali kuwaandalia jukwaa hilo kwa lengo la kuwapa elimu ya kodi.
Wanawake wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, akitembelea mabanda ya wajasiriamali Wanawake.






0 Comments