Mwakilishi wa Benki ya Dunia
nchini Bi. Xiayon Liang (kulia) akipata maelezo wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza
Ujuzi (SDF) unaoendeshwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na kuratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Wa pili
kulia ni Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi Bahati Geuzye.
Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Bi. Xiayon Liang (katikati)) akipata maelezo wakati wa ziara hiyo. Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi Bahati Geuzye.
Maonyesho kwa njia ya vitendo yakifanyika.
Na Bestina Magutu (TEA)
WAWAKILISHI wa Benki ya Dunia nchini leo wamefanya ziara ya siku moja kukagua miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoendeshwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Katika ziara hiyo, wawakilishi hao, Bi. Xiayon Liang na Bi. Innocent Mulindwa wamekagua miradi miwili (02) kati ya 81 inayotekelezwa katika awamu ya pili ya utekelezaji wa SDF ambapo wametembelea mradi wa Kuendesha na Kutengeneza Piki Piki za Magurudumu Matatu na Mawili unaotekelezwa na Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi cha Future World kilichopo eneo la Gongolamboto.
Taasisi hiyo ilipata ufadhili wa Shilingi Milioni 128.9 ambapo vijana 415 wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa kupitia ufadhili huo wa SDF.
Mradi mwingine uliotembelewa na wawakilishi hao wa Benki ya Dunia nchini ni mradi wa Mafunzo ya Mafundi wa Matengenezo ya Simu, unaoendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Chuo hiki kilichopo eneo la Kipawa kilipata ufadhili wa Shilingi Milioni 128.8 ambapo vijana 476 wamenufaika na ufadhili huo wa mfuko wa SDF.
Katika ziara hiyo wawakilishi wa Benki ya Dunia nchini wamekutana na kuzungumza na baadhi ya wanufaika wa mafunzo yaliyofadhiliwa na Mfuko wa SDF ambapo wameelezea nia ya taasisi hiyo kuendelea kufadhili mpango huo wa Serikali wa kuendeleza ujuzi kwa vijana ili kuwapa fursa ya kuajiriwa na kujiajiri wenyewe.
Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ni Mfuko unaolenga kufadhili programu za mafunzo ya ujuzi kwa wanufaika 30,000 hadi kufikia mwezi Juni 2022. Mfuko unalenga kufadhili mafunzo ya ujuzi katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni Kilimo na Kilimo - Uchumi, Utalii na Huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishati.
Katika awamu ya kwanza ya mradi ulioanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.1 wakati katika awamu ya pili Taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ambao unatekelezwa katika Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi inayofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.
0 Comments