MBUNGE WA DODOMA MJINI AISHUKURU SERIKALI KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ELIMU KUPITIA TEA

Subscribe Us

MBUNGE WA DODOMA MJINI AISHUKURU SERIKALI KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ELIMU KUPITIA TEA

Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde (mwenye fulana rangi nyekundu katikati ) akifurahia jambo na baadhi ya Waalimu wa Shule ya Msingi Medeli alipofanya ziara katika shule hiyo jana na kukagua miradi ya elimu iliyofadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Mbunge Anthony Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini akiwa darasani na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Medeli ambao walifurahia mazingira rafiki ya kusomea na kujifunzia yaliyoboreshwa kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)

Muonekano wa vyumba vya madarasa ambavyo vimejengwa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa chini ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Muonekano wa tundu la choo katika shule ya msingi Medeli iliyopo Kata ya Tambukareli jijini Dodoma, mradi uliofadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Matenki ya maji kutoka katika kisima ambacho kimechimbwa katika utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu katika shule ya msingi Medeli iliyopo Kata ya Tambukareli jijini Dodoma, mradi uliofadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde, akiwa na baadhi ya waalimu na watumishi wa Shule ya Msingi Medeli nje ya moja ya darasa lililojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).


Na Eliafile Solla - TEA


MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini  Anthony Mavunde ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa uboreshwaji wa miundombinu ya Elimu katika Jimbo la Dodoma Mjini ambapo, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imedhamini na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu yenye lengo la kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na ufundishaji.

Mavunde alitoa shukrani hizo jana wakati akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ndani ya jimbo lake na mradi mmojawapo alioutembelea ulikuwa ni Shule ya Msingi Medeli iliyopo Kata ya Tambukareli ambayo ilifanyiwa ukarabati na kuongezewa vyumba vipya vya madarasa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Katika ziara hiyo Mavunde alikagua ujenzi wa madarasa mapya, matundu ya vyoo, ukarabati wa madarasa ya zamani pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji huku akibainisha kwamba mradi huo wa jumla ya Sh. 345 Milioni umegharamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

“Ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuipa Sekta ya elimu kipaumbele na leo tunashuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa ya elimu, alisema Mavunde.’’

Mbunge huyo aliongeza kwamba, mwaka 2016 alifika katika shule hiyo na kukuta madarasa mengi hayafai na kuta zake zinakaribia kudondoka kwa kuchakaa, hivyo alitoa ahadi kwamba kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Serikali itaboresha mazingira ya shule hiyo ahadi ambayo imetekelezwa kikamilifu kila mtu ni shahidi na anaona jinsi ambavyo shule imebadilika ndani ya muda mfupi na inavutia.

‘‘Kwa furaha niliyo leo, nitawanunulia seti moja  ya kompyuta kwa ajili ya uchapishaji wa mitihani hapa shuleni ili tuwaandae vyema watoto wetu wenye mitihani ya mwisho ya Taifa waweze kufanya vizuri zaidi, alisema Mavunde’’

Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya msingi Medeli Grace Risasi aliendelea kuishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya shule ambao umepelekea kuongezeka kwa ufaulu katika shule hiyo kutokana na mazingira ya ufundishaji na usomaji kuwa rafiki tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatekeleza kazi zake chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huku ikisimamia dhamira ya kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na kuzigawa rasilimali hizo kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali ili kufadhili miradi ya elimu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa.

Post a Comment

0 Comments