SHEREHE ZA SIKU YA POSTA DUNIANI MKOA WA SINGIDA KUFANYIKA SEKONDARI YA SINGITU

Subscribe Us

SHEREHE ZA SIKU YA POSTA DUNIANI MKOA WA SINGIDA KUFANYIKA SEKONDARI YA SINGITU

Kaimu Meneja wa Posta Mkoa wa Singida Mary Kimaro akieleza mpangilio wa matukio yatakayofanyika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani Oktoba 9 mwaka huu kwa Mkoa wa Singida. 

Wafanyakazi wa Shirika la Posta Mkoa wa Singida wakiwa na furaha kwenye maadhimisho mbalimbali yanayoendelea kuelekea kilele cha Siku ya Posta Dunia Oktoba 9 mwaka huu. Maadhimisho hayo kimkoa yanatarajiwa kufanyika kwenye Shule ya Sekondari Singitu iliyopoTarafa ya Mtinko, Wilaya ya Singida mkoani hapa.

Mwonekano wa baadhi ya zawadi mbalimbali zilizoandaliwa ambazo zitakabidhiwa kwa washindi washindano la uandishi wa barua lililotangazwa na shirika hilo kuelekea kilele. 
Mwonekano wa Jengo la Posta Singida.
 Baadhi ya Vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 vikiwa vimeandaliwa tayari kwa kuvigawa kwenye siku ya kilele cha maadhimisho hayo kama sehemu ya shirika hilo kuunga mkono juhudi za serikali dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo .

Huduma zilizoboreshwa na kutumika kwa mfumo wa kidijitali zikiendelea kutolewa ndani ya ofisi za Shirika la Posta mkoani Singida kwa wateja mbalimbali kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani kwa mwaka huu.
Kazi ikiendelea.
Shamrashamra kuelekea kilele cha Siku ya Posta Duniani ndani ya ofisi Ya shirika hilo kwa mkoa wa Singida
Wananchi wakipata huduma 
Wananchi wakipata huduma 
Wananchi wakipata huduma.



Na Godwin Myovela, Singida


SHEREHE za Siku ya Posta Duniani ambazo hufanyika kila ifikapo Oktoba 9 ya kila mwaka kwa Mkoa wa Singida mwaka huu zinatarajiwa kuadhimishwa kwenye shule ya Sekondari Singitu iliyopo Tarafa ya Mtinko Wilaya ya  Singida mkoani hapa.

Imeelezwa sababu ya kufanyika shuleni hapo ni kutokana na shule hiyo kuibuka kinara kwa kutoa idadi kubwa ya wanafunzi waliojitokeza kushiriki shindano la uandishi wa barua katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Posta mwaka huu.

Sambamba na hilo, katika maadhimisho hayo timu ya wafanyakazi wa shirika hilo itaambatana na jopo la wataalamu wa afya ambao pamoja na mambo mengine watajikita katika kutoa elimu juu ya ugonjwa wa COVID 19 zoezi ambalo litakwenda sanjari na ugawaji wa vifaa mbalimbali vya kujikinga, ikiwa ni sehemu ya shirika hilo kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Kaimu Meneja wa Posta Mkoa wa Singida, Mary Kimaro alisema pia maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu isemayo ‘Ubunifu kwa Posta Endelevu’ ambayo kitaifa yanatarajia kufanyika jijini Dodoma, shirika hilo pamoja na mambo mengine litajikita zaidi katika kujitangaza na kueleza umma juu ya maboresho yake makubwa ya kihuduma yanayoendelea kutolewa kwa sasa kwa kuzingatia mifumo ya kidijitali ikilinganishwa na siku za nyuma.

“Lengo hasa la kuadhimisha kwenye shule hii ni kuongeza hamasa kwa shule na washiriki wengine kuiga mfano huo na kufanya vizuri zaidi kwenye maadhimisho ya mwaka utakao fuata…Posta kwa sasa tupo kidijitali zaidi nitoe wito kwa umma kuzidi kutembelea ofisi za shirika letu na kutuunga mkono kwa kujipatia huduma zetu mbalimbali za kidijitali zilizoboreshwa.” Alisema Kimaro.

Shirika hilo kwa sasa pamoja na mambo mengine linatoa huduma za kidijitali za Duka Mtandao, Intaneti Café, tuna mfumo madhubuti wa kufuatilia barua au kifurushi kilichotumwa kupitia mtandao kujua kimefikia wapi au kimepokelewa na nani.

Pia Kimaro alieleza kuwa Posta ndani ya Singida kwa kuzingatia mifumo ya kasi ya TEHAMA linaendelea kusafirisha barua kwa njia ya haraka (EMS) ndani na nje ya nchi, usafirishaji mizigo mikubwa, kutoa huduma ya masanduku ya barua ikiwemo kwa kutumia TEHAMA ya Posta Kiganjani na huduma ya Uwakala wa Fedha.

Pia kwa mujibu wa Kaimu huyo Meneja shirika hilo pia lina magari ya uhakika kwa usafirishaji wa vifurushi vya hadi tani 30 hivyo watanzania wanakumbushwa kuchangamkia fursa hiyo ya  usafirishaji mizigo kwa njia ya magari kwa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma kwa kuingia na kutoka Singida kila siku kuanzia majira ya saa 10 jioni.

“Magari yetu ya Dar es Salaam hupitia miji ya Morogoro, Dodoma na Manyoni, na yale ya Mwanza hupitia njia ya Shinyanga huku yale ya Kigoma hupitia miji ya Nzega, Tabora, Urambo hadi Kigoma,”alisema Kimaro. 

Tangu kuanzishwa kwake kwa Sheria ya Bunge Namba 19 ya Mwaka 1993 nakuanza kazi rasmi Januari Mosi, 1994 shirika hilo hatua kwa hatua limeendelea kufanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma zake mbalimbali, zikiwemo huduma ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya ‘Posta Cash’, Uwakala wa Bima, Huduma za uuzaji wa hisa za makampuni mbalimbali na huduma za Bodi ya Mikopo na Baraza la Mitihani.

 

Post a Comment

0 Comments