Na Veronica Simba, REA - Mtwara
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala ametoa pongezi kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutokana na kazi nzuri inayofanyika kupeleka umeme vijijini.
Alitoa pongezi hizo ofisini kwake wakati akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, waliokuwa katika ziara ya kazi jana wilayani humo.
“Tunawapongeza na kuwashukuru REA kwa kushirikiana na TANESCO. Tunatambua kazi kubwa mnayoifanya tunafarijika sana,” alisema Kanali Sawala.
Aidha, Mkuu wa Wilaya alipongeza kasi ambayo REA imeanza nayo katika kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili wilayani humo na kusisitiza kuwa iendelee hivyo ili vijiji vilivyosalia vipate umeme kwa wakati uliopangwa.
Vilevile, alipongeza maelekezo yaliyotolewa na Uongozi wa REA kwa mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani humo, kuandaa Mpango Kazi na kuuwasilisha katika ofisi yake, ofisi ya mbunge, diwani na serikali za mitaa akisema kuwa itarahisisha ufuatiliaji wa utendaji kazi hatua kwa hatua.
Akifafanua zaidi, Kanali Sawala alisema kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kinachofanyika, namna watakavyonufaika na mradi husika na kwa wakati gani kwani kwa namna hiyo watatoa ushirikiano nzuri katika utekelezaji wake.
Pia, alitoa rai kwa Wakala kutekeleza kwa haraka kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vya wilaya hiyo vilivyoko mpakani mwa nchi ili kuwezesha uimarishaji zaidi wa ulinzi na usalama wa nchi.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa REA walimtembelea Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Yusuf Nannila na kuzungumza naye kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM hususan katika sekta ya nishati vijijini.
Mwenyekiti huyo wa CCM alieleza kuwa Uongozi wa Chama unafarijika kuona maelekezo yaliyotolewa katika Ilani kuhusu sekta ya nishati vijijini, yanatekelezwa kwa vitendo.
“Leo tunashuhudia kwamba Ilani yetu haikuwa maneno matupu bali ni matendo kama inavyojidhihirisha sasa,” alisema.
Hata hivyo, Nannila alitoa wito kwa watendaji wa serikali kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili vijiji vyote vifikiwe na umeme ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba, 2022 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya CCM.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Saidy, walimhakikishia Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa CCM kuwa watatekeleza maagizo yote waliyowapatia.
Walieleza kuwa REA imejipanga kuhakikisha inatekeleza azma ya serikali kufikisha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwishoni mwa Desemba, 2022.
Aidha, walieleza kuwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini, wameshajulishwa kuwa hakutakuwa na ongezeko la muda wa kukamilisha miradi hiyo, hivyo wanapaswa wajipange kuhakikisha miradi inakamilika kwa muda uliopangwa.
Wakili Kalolo alimwomba Mwenyekiti wa CCM kufikisha salamu za shukrani kutoka REA kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini na kwamba REA inaahidi haitamwangusha.
Akifafanua zaidi kuhusu utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mkoani Mtwara, Mhandisi Saidy alieleza kuwa umelenga kuvifikishia umeme vijiji 402 vilivyosalia.
Mwenyekiti Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wako katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.
0 Comments