VIJANA WAASWA KUINGIA KWENYE UFUGAJI NYUKI KWA KUWA UNA FAIDA KUBWA

Subscribe Us

VIJANA WAASWA KUINGIA KWENYE UFUGAJI NYUKI KWA KUWA UNA FAIDA KUBWA

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mathayo Masselle akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa nyuki wa kisasa kwa vijana 1500 wa Wilaya za Ulanga na Malinyi. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira.
Kaimu Katibu Tawala  Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira akitoa salamu za mkoa huo wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa ufugaji nyuki kwa vijana.
Meneja Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, Caroline Malundo akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa (TFS) Kamishina, Profesa Dos Santos Silayo kwenye uzinduzi huo.
  Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya  ACLA HONEY,  Giovanni Nguvu akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo.
Afisa Maliasili Mkoa wa Morogro Manjiva Nzunda akitoa taarifa ya ufugaji nyuki na mipango ya uhifadhi maliasili kwa mkoa huo.
Mmoja wa Wanufaika wa mradi huo Faraji Mbowela akizungumza kwa niaba ya vijana wanufaika wa mradi huu kutoka Wilaya ya Malinyi.

ViViongozi mbalimbali wakifuatilia maelezo ya ufugaji bora wa nyuki na kujionea vifaa vya kisasa vya ufugaji vilivyotolewa kwa ajili ya mradi huo wa Acla Honey.

Viongozi mbalimbali wakifuatilia maelezo ya ufugaji bora wa nyuki na kujionea vifaa vya kisasa vya ufugaji vilivyotolewa kwa ajili ya mradi huo wa Acla Honey.
Uzinduzi ukiendelea.
Uzinduzi ukiendelea.
 


Na Amina Hezron – Morogoro.

VIJANA kote nchini wametakiwa kujishughulisha na biashara ya ufugaji bora na wa kisasa wa nyuki kutokana na ufugaji huo kutokuwa na gharama kubwa lakini kuwa na faida kubwa, soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi,  Mathayo Masawe  wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa nyuki wa kisasa kwa vijana unaotekelezwa katika wilaya ya Ulanga na Malinyi,unaoendeshwa  na kampuni ya ACLA HONEY Chini ya Programu ya  kuwajengea ujuzi  vijana (SET) inayotekelezwa na shirika la Swisscontact kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo la Uswis (SDC).

“Kwa mujibu wa takwimu ambazo nimepewa hapa nimesikitika kidogo kwamba Malinyi tuna mizinga 144 tuu,Niwaambie ndugu zangu wa Malinyi hiyo mizinga 144 alitakiwa kuwa nayo mtu mmoja tu,maana kuna watu wana mizinga mpaka 2000 mtu mmoja tu.” alieleza Masselle.

Aliongeza “ kama hawajawaambia vizuri kazi yako ni ndogo ukishakuwa na mziga wako kauweke pale kaendelee na shughuli zako za shamba wala hutatakiwa kuamka asubuhi kumtafuta nyuki maana wenyewe wanatafuta nyumba akifika pale ataingia na atakutengenezea asali utaivuna mara tatu kwa mwaka, kwahiyo nendeni mkafanye ujasiliamali wa nyuki”.

Ameongeza kuwa watu wengi wametajirika kupitia ufugaji wa nyuki ndio maana kwenye mradi huu wamechukua vijana kuanzia miaka 14 hadi 24 ambayo bado wanakua, lakini pia wazazi mkajifunze kutokana na hawa vijana wetu na nyinyi mkaweke mizinga na wakati mwingine sio lazima ukaweke msituni bali ni kwenye eneo fulani kitaalamu maana nyuki wanatembea kila siku kutafuta nyumba.

“Niwaombe ndugu zangu wa Malinyi tunapozipata fursa tuzichangamkie maana najua huwa tunachelewa sana kukubali kuzichangamkia lakini nafahamu tunapozichangamkia huwa tunazichangamkia kwelikweli na niwaombe mpeleke taarifa hizi kwa wale ambao hawapo na wenzetu wa shirika la ACLA HONEY tayari wamewafundisha vijana 1000 kwenye wilaya yetu” alisisitiza”.

 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka vijana kuacha kukimbilia mjini kuendesha bodaboda, kupiga debe stendi na kufanya biashara nyingine zisizo na tija badala yake wabaki vijiji ambapo kuna fursa nyingi na zenye tija kubwa kwa Maisha yao na familia zao.

“Ufugaji wa nyuki ni fursa nzuri sana kwa vijana na kwa mkoa wa Morogoro tunafuga nyuki kwenye Halmashauri zetu zote ambapo tuna mizinga takribani 14,000 hivyo unaweza kuona namna watu wanavyochangamkia hii fursa lakini kwa Halmashauri hii ya malinyi kuna mizinga 144 kati ya hiyo 14,000 hivyo utaona kwa upande huu ufugaji wa nyuki sio mkubwa” alibainisha Dkt.Rozalia.

Kaimu katibu tawala huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema mradi huu unatarajia kuwafikia vijana 1500 katika Wilaya zote mbili na vijana wengine watakapoona faida wanazozipata vijana hao walio ndani ya mradi nao watahamasika na kuanza kufuga nyuki na kulina asali na kujipatia faida.

Alisema Serikali ina wajali sana vijana wa nchi hii ndio maana ikaanzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya asilimia nne isiyo na riba kupitia kila halmashauri hivyo ni vizuri sasa wakaanzisha vikundi vya ufugaji nyuki na kuziomba fedha hizo katika kutengenezea mizinga hivyo ni vyema wakaonana na Wakurugenzi wa Hamshauri zao.

“Tayari kuna kiwanda kimekuja kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kinahitaji asali kutoka Mkoani kwetu lakini kiasi wanachotaka Mkoa wetu bado haujafikia uwezo wa kuzalisha asali hiyo kutokana na kuwa na wafugaji wachache, hivyo mnaweza kuona soko lipo kubwa sana hivyo changamkeni tunufaike na rasilimali nyuki” aliwahakikisha Dkt. Rozalia.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa (TFS) Kamishina, Profesa Dos Santos Silayo, Meneja Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, Caroline Malundo alisema wao kama wasimamizi wa Misitu wanaahidi kushirikiana na kampuni hiyo ya Acla Honey katika kufanikisha mradi huu ambao una faida kubwa kwa maisha ya vijana na Taifa ili uweze kufanya vizuri na kuenezwa nchi nzima.

Alisema kuwa Tanzania ina mazingira mzuri sana ya ufugaji wa Nyuki na hii ni elimu ambayo wote tunapaswa kuijua na kwa takwimu Tanzania ina fursa ya kuzalisha asali tani 138,000 lakini tunazalisha tani 34,000 tu na fursa ya kuzalisha  tani 92000 za nta  wakati tunazalisha tani 1843 tu.

“Tanzania ina hekta Milioni 48.1 ambazo zinafaa kwa uzalishaji wa asali na takribani asilimi 90 ya shughuli za ufugaji nyuki zinafanywa kwa kutumia mbinu za asili kama vile utengenezaji wa mizinga kwa kutumia magamba ya miti na hii ndio imekuwa sababu kubwa ya uzalishaji mdogo wa asali nchini ikilinganishwa na uweo tulionao hivyo kuja kwa shirika hili la ACLA HONEY kutasaidia kuboresha mizinga,Uvunaji na uzalishaji wa asali” alifafanua  Malundo.

Aliongeza “Wakala wa huduma za Misitu Tanzania TFS pia anasaidia kutafuta masoko ya asali  kitaifa na kimataifa na kwamba hatutaki  uishie hapa Tanzania  bali tuunze nchi za nchi nje ili kupata fedha za kigeni na TFS imekuwa ikifanya utafiti kupitia wataalamu ili kubaini ubora wake na tayari majibu yameonesha Tanzania ina asali bora kwa kuuzwa nchi ya nchi za nje pia”.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ACLA HONEY,  Giovanni Nguvu amesema kampuni hiyo ambayo imetokana na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia taasisi ya SUGECO ina mashamba kwenye Mikoa saba ya Tanzania yenye mizinga 7,000 na kampuni yao huzalisha asali tani zaidi ya 25,000 kwa mwaka na soko kubwa la asali yao ni nje ya nchi.

Alisema kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo na uaminifu umekuwa ukitekeleza miradi mbalimbali nchini na sasa wamepata ufadhi wa kutekeleza mradi huu ambao utahusisha wilaya mbili za Malinyi na Ulanga na utawafikia vijana 1500 moja kwa moja wenye umri kati ya 14 hadi 24 na kati yao 5000 wakitoka wilaya ya Ulanga na 1000 wakitoka Wilaya ya Malinyi.

“Mradi huu una malengo ya kukuza kipato cha kaya na kuongeza lishe kupitia ufugaji wa nyuki wa kisasa ambapo pamoja na wanufaika kuunganishwa kwenye vikundi na kupatiwa mafunzo lakini pia watapewa mizinga ya kisasa ya ufugaji wa nyuki,vifaa vya kulina asali na mazao mengine ya nyuki na kuhakikishiwa soko la mazao yote ya nyuki yatakayozalishwa” alibainisha Nguvu.

Akiongeza “Mafunzo hayo pia yatakwenda mbali zaidi kwa kuwafundisha mbinu bora za kuongeza thamani mazao yatokanayo na nyuki kama vile kutengeneza Mishumaa,ving’arisha viatu, ving’arisha Midomo, Mvinyo pamoja na bidhaa zingine nyingi”.

Amesema Mradi huo kwa sasa upo kwenye hatua za majaribiokwa kipindi cha miezi saba  kutoka mwezi wa nane  hadi wa tatu mwakani na pindi mfadhili atakaporidhishwa na matokeo ya utekelezaji ya mradi awamu kuu ya miaka minne ya  Mradi itaanza Mwezi Mei 2022 hadi mwezi Aprili 2026.

Akizungumza kwa niaba ya wajana wanufaika wenzake wa mradi huu, Faraji Mbowela ameshukuru kwa Shirika hilo kupeleka mradi huo kwenye wilaya yao kwani utawakwamua vikaja wengi wanaokaa vijiwemo na wengine kujishughulisha na vitendo hasi kwenye jamii kama vile wizi,uvutaji wa bange.

“Kilichonivutia ni maelezo ya ufugaji wa nyuki na namna biashara hiyo inavyofanyika kwa urahisi tofauti na nilivyokuwa nafahamu lakini pia kuna maslahi makubwa hasa kama mimi natarajia kuwa na familia yangu huko mbeleni hivyo nitahakikisha nafanya kazi kwa bidii kwa kuongeza mizinga kila mara ili nipate asali nyingi zaidi na kuongeza kipato changu” alisema Mbowela.

 Mradi wa ufugaji wa nyuki kisasa kwa vijana katika wilaya ya Ulanga na Malinyi (CHIBS) unaendeshwa na kampuni ya ACLA HONEY Chini ya Mradi wa kuwajengea ujuzi vijana Tanzania  (SET) unaotekelezwa na shirika la Swisscontact kwa Ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).                                                        

Post a Comment

0 Comments