MANISPAA SINGIDA YATUMIA MIL.701/- KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Subscribe Us

MANISPAA SINGIDA YATUMIA MIL.701/- KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe akizungumza na fundi wakati akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mtipa kinacho jengwa Kitongoji cha Mwampembee Kata ya Mtipa katika ziara ya siku moja aliyoifanya leo Februari 17, 2023.

..................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MANISPAA ya Singida imetumia Sh.Milioni 701.6  kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo fedha ambazo zimetokana na mapato ya ndani.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe akizungumza leo (Februari 17) baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mtipa kinacho jengwa Kitongoji cha Mwampembee Kata ya Mtipa, alisema  fedha hizo zilitumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hadi kufikia Disemba 2022.

Akitoa mchanganuo wa jinsi fedha hizo zilivyotumika alisema  Sh. Milioni 5.8 zilitumika kuwalipa wananchi wanne fidia ya utwaaji eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.

Alisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ni Sh.500 Milioni lakini zilizopokelewa ni Sh.170.1 na kuwa ujenzi upo hatua ya boma kwa majengo ya OPD na Maabara pamoja na kichomea taka.

Lupembe alisema mambo mengine yaliyofanywa na manispaa hiyo kutkana na fedha hizo ni ununuzi wa magari mawili ya kuzoa taka yenye thamani ya Sh.Milioni 220 pamoja na kununua kifaa cha kupimia ardhi Sh.Milioni 50 na ujenzi wa machinjio inayojengwa eneo la N’gaida kwa gharama ya Sh.Milioni 120.

Aidha, Lupembe alisema halmashauri hiyo imetoa fedha asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya vikundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ambapo fedha zilizopokelewa ni Sh.Milioni 222.5 ambapo vikundi 213 viliomba mkopo lakini vilivyokidhi vigezo ni 81 tu.

Lupembe alitaja matumizi ya fedha hizo kuwa ni ukamilishaji wa nyumba ya mtumishi inayojengwa eneo la Veta ambapo fedha zilizotengwa ilikuwa ni Sh.Milioni 29 lakini zilizopokelewa ni Sh.Milioni 10 ambapo ujenzi wake unaendelea.

Alisema kazi nyingine iliyofanyika kutokana na fedha hizo ni ujenzi wa matundu manne ya vyoo katika Shule ya Sekondari Mahalu ambao ulitumia Sh.Milioni 8.8  na kuwa ujenzi wake umekamilika.

Lupembe alitaja matumizi mengine ya fedha hizo kuwa ni ununuzi wa gari aina ya Land Cruiser ambalo limenunuliwa kwa Sh.Milioni 18.1 pamoja na ununuzi wa viti 74 kwa ajili ya ukumbi wa Manispaa hiyo kwa gharama ya Sh.Milioni 20.

Alitaja kazi nyingine iliyofanyika ni kutengeneza viti na meza 60 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Unyianga kwa gharama ya Sh.Milioni 3.3 na ukamilishaji wa choo cha Zahanati ya Unyianga kwa gharama ya Sh.Milioni 4.3 ambaoujenzi wake upo hatua za mwisho.

Pia Lupembe alisema kuwa kazi nyingine iliyofanyika ni upandaji wa miti 812, 153 kwa gharama ya Sh.Milioni 1.9 na ukarabati wa kituo kikuu cha mabasi na ujenzi wa ofisi ndogo ya wakusanyaji wa ushuru kwa Sh.Milioni 7.

Lupembe aliongeza kuwa kazi nyingine iliyofanyika ni utengenezaji wa mtambo wa kuzolea taka ulioharibika kwa zaidi ya miaka miwili ambao umegharimu Sh. Milioni 16, ununuzi wa sare za jeshi la akiba ambazo zilinunuliwa kwa Sh.Milioni 2.8 pamoja na shughuli wa upimaji wa maeneo mbalimbali kazi iliyogharimu Sh. 635,000.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe akizungumza na mafundi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Mtipa.
Muonekano wa jengo la OPD.
Muonekano wa jengo la OPD.
Muonekano wa jengo la Maabara.
Mkazi wa Kijiji cha Mtipa, Juma Kilanga akifurahia ujenzi wa kituo hicho ambacho kikikamilika kitawapunguzia adha wananchi wa eneo hilo ya kutembelea umbali mrefu wa kufuata tiba maeneo mengine.
Msimamizi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, Joseph Linje akizungumzia ujenzi wa kituo hicho ambapo ameahidi kukamilika baada ya miezi mitatu ijayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtipa, Musa Bayo  akizungumzia ujenzi wa kituo hicho ambapo aliwaomba wananchi kujitokeza kushiri shughuli za ujenzi wa kituo hicho.

Post a Comment

0 Comments