Mchungaji wa Kanisa la Moravian Kusini Kati Tanzania Parishi ya Singida Mjini, Yona Mbogo (kushoto) akiongoza maombi ya kuwaombea wafanyakazi kuelekea sherehe za Mei Mosi 2023 zitakazofanyika kesho duniani kote katika maombi yaliyofanyika leo Aprili 30, 2023 wakati wa siku ya uimbaji iliyofanyika kanisani hapo.
.....................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
KANISA la Moravian Kusini Kati Tanzania Parishi ya Singida Mjini kuelekea
Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi 2023 limewaombea wafanyakazi wote nchini ili
wawe na afya bora na kuweza kufanyakazi zao mbalimbali kwa ajili ya kuinuka
kiuchumi na taifa kwa ujumla.
Ombi hilo limetolewa na Mchungaji wa kanisa hilo, Yona Mbogo wakati
akiongoza maombi maalum ya kuwaombea wafanyakazi katika siku ya uimbaji
iliyofanyika leo Aprili 30 katika kanisa hilo lililopo Mwenge Manispaa ya
Singida.
"Siku ya leo tupo katika ibada hii kwa ajili ya kuwaombea wafanyakazi
wote walio ajiriwa, kujiajiri, wakulima, wafanyabiashara, sekta binafsi na
wengine wote wanaofanya kazi kwa mikono yao ili wapate baraka za mafanikio
kutoka kwa Mungu kuelekea kilele cha Sikukuu ya wafanyakazi itakayofanyika
duniani kote kesho Mei Mosi, 2023," alisema Mchungaji Mbogo.
Alisema pamoja na kuwaombea wafanyakazi hao pia wanawaombea wale wote ambao wanachangamoto ya kutokuwa na kazi ambao wanazungka na vyeti vyao ili wapate kazi na wale wenye kazi warudi kwenye madhabahu ya Mungu kumtolea sadaka baada ya kupata mafanikio yaliyotokana na kazi zao" alisema Mbogo.
Mchungaji Mbogo aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii kwa uweza wa
Mungu na si kutumia nguvu za giza, kufanya matambiko, uchawi, chuma ulete na
mambo mengine yanayofanana na hayo kwa lengo la kuzuia mafanikio ya watu
wengine.
Aidha, Mchungaji Mbogo alisema watu wote wanaoharibu kazi, uchumi na maisha
ya watanzania kwa namna mbalimbali
wapingwe kwa nguvu zote kwani huo sio mpango wa Mungu.
Mchungaji Mbogo aliwataka wafanyakazi wote na kila mmoja kwa shughuli
anayoifanya wakiwemo wanafunzi baada ya sikukuu hiyo kuendelea kufanya
kazi na kusoma kwa bidii ili kuliinua
taifa kiuchumi kwani hata biblia
imeeleza asiyefanya kazi na asile.
Katika siku hiyo ya uimbaji kwaya mbalimbali na waimbaji mmoja mmoja walipata fursa ya kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu na kusifu.
0 Comments