Na Mwandishi Wetu, Singida, Singida
MKOA wa Singida umepanga kusherehekea maadhimisho
ya sherehe za miaka 59 ya muungano ambayo kilele chake kitafanyika wilayani
Manyoni kwa kufanya usafi katika maeneo yote ya Mkoa ikiwamo barabara kuu ya
Singida-Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba,
akizungumza na waandishi wa habari jana alisema usafi huo ambao utawashirikisha
wananchi pia utafanyika katika ofisi za serikali, taasisi mbalimbali,
shule,vyuo na maeneo ya masoko.
Alisema kazi nyingine zitakazofanyika ni uzinduzi
wa miradi ya maendeleo katika hospital ya Wilaya ya Manyoni ambapo jengo la
wagonjwa la dharula litazinduliwa na kutembelea mradi wa ujenzi wa daraja
katika barabara ya Kintinku-Singida hadi Malendi.
Serukamba alitaja shughuli nyingine zitakazofanyika
ni kufanya mdahalo kuhusu muungano,kufanya bonanza la michezo,kufanya mahojiano
na wazee maarufu wanaojua historia ya Mkoa wa Singida na kuwaeleza wananchi
mafanikio ya maendeleo ndani ya muungano.
Alisema katika kipindi cha miaka 59 ya muungano
kumekuwa na mafanikio mengi kwa wananchi wa pande zote za muungano ambayo ni
pamoja na suala la ulinzi na usalama, kisiasa na mwingiliano wa kijamii.
Mkuu wa Mkoa alisema katika suala la ulinzi
limefanikiwa kwa asilimia 100 hasa
ulinzi wa mipaka ya nchi hali ambayo imesaidia kupiga hatua kwenye maeneo ya
kijamii,kisiasa na kimahusiano ya kimataifa.
"Kama sio muungano wetu eneo la ulinzi na
usalama lingekuwa na changamoto nyingi tofauti na sasa ambapo sasa hivi Jeshi
letu la ulinzi ni moja kwa pande zote,hali hii imeleta utulivu na uimara wa
jamii zote mbili za muungano," alisema.
Serukamba alisema katika suala la kisiasa alisema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikija kujifunza Tanzania hasa katika suala la makabudhiano ya madaraka kutoka awamu ya kwanza hadi sita bila rapsha tofauti na nchi nyingine.
0 Comments