Prof. Reuben Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) kwa upande wa Tanzania wakati akieleza matokeo ya jumla ya Mradi mbele ya wadau wa mazao yaliyokuwa yanafanyiwa utafiti na mradi huo.
Na Amina Hezron, Kilimanjaro.
Imebainika kuwa kutokuongeza thamani
kwa baadhi ya mazao na kutokidhi vigezo vinavyowekwa kwenye Soko la dunia na
wanunuzi wengine hususani nchi za Ulaya ndio sababu kuu ya Mazao mengi ya
wakulima nchini kutosafirishwa kuuzwa nje na kupata faida kubwa.
Hayo yamebainishwa na Prof. Reuben
Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na
Mazingira (TRADE Hub) wakati akieleza matokeo ya jumla ya Mradi huo unaotekelezwa
na Chuo Kikuu cha Sokoine ha Kilimo (SUA) nchini Tanzania na kwenye nchi zingine 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil.
“Wahitaji wanunuzi wa bidhaa zetu wanaenda wanabadirika wakiweka
vigezo kanuni na sheria mbalimbali zinazotakiwa kuzingatiwa wakati wa
uzalishaji ikiwemo uzalishaji unaolinda mazingira, haki kwa wafanyakazi kwenye
kuzalisha zao hilo na mengine mengi ambayo ukiangalia kwa nchi yetu na nchi
nyingi zinazoendelea hiyo inakuwa kikwazo kikubwa hivyo lazima nchi yetu
tujipange kutimiza vigezo hivyo ili tunufaike”,alieleza Prof.
Kadigi.
Mhadhiri na Mtafiti huyo Mwandamizi
wa Uchumi Kilimo amesema masharti hayo hayaishii kwenye maneno tu kwa kusema
bali wanakuja na mifumo thabiti ya kufuatilia kujua kama kweli kile
wanachouziwa kutoka kwenye nchi mbalimbali duniani kinafuata masharti yao yote
waliyoyaweka.
Aidha amesema kufuatia changamoto
hiyo nchi nyingi zinashindwa kufikia vigezo hivyo na kupelekea pale
wanapokwenda kuuza kwenye mataifa hayo mazao na bidhaa zao zinakuwa na
ushindani mkubwa kwakuwa kuna watu wanaojitangaza zaidi huko na wameweza
kukidhi viwango hivyo vinavyotakiwa na soko.
Mtafiti huyo Mkuu wa Mradi wa TRADE
HUB amesema jitihada za pamoja zinatakiwa kati ya Serikali,Wakulima na
Makampuni makubwa ambayo yanasafirisha Mazao nje ya nchi kuwakingia mgongo
wakulima wa Tanzania kwa kuwasaidia kufikia vigezo kwakuwa ili kutambuliwa pia
kuna gharama kubwa ambazo wakulima wadogo na vyama vya ushirika haviwezi kumudu.
Akizungumzia changamoto nyingine ya
kutoongeza thamani kwa mazao kabla ya kusafirisha kwenda nje ya nchi kwa
kutolea mfano zao la Kahawa amesema asilimia kubwa Tanzania inasafirisha kahwa
ghafi (Green Coffee) wakati zipo teknolojia nyingi za kukaanga Kahawa na
kuiongezea thamani hali inayowafanya wakulima kupata hela kidogo huku wanaoongeza
thamani kupata fedha kuliko mkulima.
“Nimefanya utafiti kuangalia zao la
Kahawa duniani nimeona kuwa nchi nyingi zinauza Kahawa ghafi zinapata fedha
kidogo sana na inanunuliwa na nchi ambayo haina hata mti mmoja wa Kahawa yaani
hawalimi kabisa na kisha wanaongeza thamani tena ndogo ambayo ingeweza fanyika
hapa nchini lakini wanapata faida mara tatu zaidi kuliko sisi au mkulima
aliyelima”, alieleza Prof. Kadigi.
Hivyo ameiomba Serikali katika
jitihada kubwa inazozifanya katika kuinua kilimo na kufufua zao la Kahawa kuona
namna ya kusaidia eneo hilo la uongezaji thamani kwa Kahawa ya wakulima wa
Tanzania ili waweze kupata faida kubwa na kuona thamani ya zao hilo ambalo
wakulima wengi waliamua kuliacha kutokana na tatizo la bei.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu kutoka
Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) katika Kituo cha Dunia cha
Ufatiliaji wa Uhifadhi (WCMC) Prof. Neil Burgess amesema mradi
huo unafanya utafiti kuangalia Biashara, Maendeleo na Mazingira ya mazao ya
Kilimo na Wanyamapori katika nchi washiriki.
“Huu ni mradi wa utafiti wa kimataifa
unaoangalia sera za kimataifa za biashara, Usimamizi wa bishara na Kanuni za
biashara lakini pia faida na hasara za
kanuni zilizowekwa kimataifa kwenye biashara mfano mzuri ni hizi za Umoja wa
Ulaya ambazo zinaonekana kuathiri nchi nyingi zinazoendelea”, alifafanua Prof.
Burgess.
Amesema kuwa kwa Tanzania kazi
kubwa imefanywa na watafiti wa SUA kupitia Mradi huo kwa miaka mitatu na sasa
mwaka wa nne wanamalizia kwa kuendesha Warsha ya uhamasishaji kwa wadau pamoja
na kutengeneza muelekeo wa pamoja wa namna ya kuzalisha na kufanya biashara
kimataifa sambamba na biashara uendelevu ya Nyama Pori.
Mtafiti huyo mkuu amesema kazi
field na kukusanya taarifa zimemalizika na sasa wameweka nguvu katika kuandika
matokeo kwa kufanya utambuzi wa kina ili kupata kitu ambacho kitakuwa na faida
kutumika kwa taifa, Watunga sera na Wakulima ambao wanaguswa na mifumo
mbalimbali ya uzalishaji.
Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana Taasisi zingine zaidi ya 50 duniani na kutoka katika nchi 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil na kufadhiliwa na Mfuko wa Utafiti wa Changamoto za Kidunia wa Serikali ya Uingereza (UKGCRF) na Mfuko wa Pamoja wa Utafiti na Ubunifu (UKRI).
Wadau wakifuatilia matokeo wakati wa warsha hiyo.
Wadau hao wakifuatilia matokeo wakati wa warsha hiyo.
0 Comments