Na Dotto Mwaibale, Singida
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinawaomba Watanzania kuutumia mwaka
2024 ambao umewekwa wakfu kwa ajili ya uwekezaji hapa nchini hivyo wasiache
upite bila ya kuchangamkia fursa hiyo adhimu.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani wa kituo hicho
Felix John wakati akizungumza na
waandishi wa habari wa Mkoa wa Singida Januari 15, 2024 kwenye kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani.
John alisema lengo la kampeni hiyo ni utekelezaji kwa vitendo wa ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kuiunga mkono kampeni hiyo iliyozinduliwa rasmi Septemba 25, 2023 na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam.
Alisema kampeni hiyo moja ya lengo lake kuu ni kubadilisha fikra zilizodumu
kwa muda mrefu miongoni mwa Watanzania
ambao wanaposikia dhana ya uwekezaji wanafikiri inawalenga wageni au wazungu
na ndio maana imeanzishwa ili nao waweze kuwekeza katika miradi
mbalimbali na kushiriki kuinua uchumi wao na nchi kutokana na fursa zilizopo
kwenye maeneo yao.
Alisema kujitokeza kwao katika uwekezaji ni kuunga mkono adhima ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtaka kila mtanzania kushiriki katika uchumi wa
nchi kupitia uwekezaji.
John alisema Waziri wa Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo alisema hivi sasa asilimia 46 ya
uwekezaji hapa nchini ni wa wazawa na asilimia 29 ni wageni na kuwa miradi
inayofanywa kwa ubia kati ya watanzania na wageni ni asilimia 26..
Aidha, John alisema maboresho yaliyofanywa na Rais Samia ya ubadilishwaji
wa sheria na kupunguza viwango vya mtaji imesaidia kuongeza idadi ya
wawekezaji wanaosajiliwa TIC baada
kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022 ambayo
imepunguza thamani ya mtaji unaohitajika kwa mwekezaji wa ndani kutoka Dola za
Kimarekani 100,000 hadi 50,000 kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani.
Alisema sheria hiyo namba 10 ya 2022 inatambua wawekezaji mahiri nakupewa
vivutio vya uwekezaji na kuwa wale wenye sifa wanapewa misamaha ya kodi kwa
kuwa ndani ya kipengele hicho cha umahiri.
Alisema hivi sasa suala zima la uwekezaji limebadilika kwa kasi kubwa na
Rais Samia Suluhu Hassan kuonekana ni kinara na namba moja kutokana na nchi
kuwa na sheria hiyo ambayo inawavutia wawakezaji wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alisema TIC kuanzisha kituo cha
utoaji huduma mahali pamoja ‘ One Stop Facilitation Centre’ ni hatua nzuri
katika kumsaidia mwekezaji kwani akifika TIC atapata huduma zote za usajili
kutoka taasisi zinazohusika kama TBS na TRA hivyo kumpunguzia mlolongo
uliokuwepo hapo zamani wa kufuata huduma hizo kwenye taasisi hizo.
Msimamizi wa Kiwanda cha Wild
Flower,Grains and Oil Mill Project, Jamal Juma, alisema kiwanda hicho kitakapo
kamilika ujenzi wake kitatoa ajira za kudumu 190 na za muda mfupi zitakuwa
zaidi ya 400 na kwamba wakulima zaidi ya 10,000 wa Mkoa wa Singida watanufaika
na kiwanda hicho chenye uwekezaji wa zaidi ya Sh.bilioni 56.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Khalid Ally Omary (Shullu), kupitia Mkuu wa Mkoa wa
Singida, Peter Serukamba alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan awe mgeni rasmi na
kukifungua kiwanda hicho mara ujenzi wake utakapo kamilika.
Naye Meneja wa TIC Kanda ya Kati, Venance Mashiba alipongeza kampuni hiyo
kwa kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati kwani kinakwenda kuinua
uchumi wa nchi hasa baada ya kuzingatia ushauri uliokuwa ukitolewa na TIC.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi upande wa Viwanda na Biashara Mkoa wa Singida,
Lucas Mkuki aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza Mkoa wa Singida kwani
Jiografia yake inaufanya iwe kivutio kikubwa na kuwa na miundombinu mizuri ya
barabara pamoja na maeneo ya kilimo ya kutosha.
Mkurugenzi wa Shule za Lake, John Augustino ambaye ni mmoja wa wakezaji Mkoa wa Singida aliishukuru sana TIC kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwake hadi kufikia hatua hiyo kubwa aliyonayo hasa katika msaada ya vifaa vya ujenzi, magari na ushauri ambapo aliwaomba wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida kwenda kusajili biashara zao TIC ili zitambulike.
Meneja wa TIC Kanda ya Kati, Venance Mashiba, akizungumza katika kampeni hiyo.
Msimamizi wa kiwanda hicho Jamal Juma akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Mkurugenzi wa Shule za Lake, John Augustino, akisubiri kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu uwekezaji wa shule yake.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule za Lake.
Wanafunzi wa Shule ya Lake wakiwa darasani.
0 Comments