CDF YATANGAZA MRADI MPYA WA KUPAMBANA NA UKATILI WA KINGONO WILAYA YA MPWAPWA

Subscribe Us

CDF YATANGAZA MRADI MPYA WA KUPAMBANA NA UKATILI WA KINGONO WILAYA YA MPWAPWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mradi mpya wa kupambana na ukatili wa kingono wilayani Mpwapwa Februari,  28, 2024.

...................................

Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa

SHIRIKA  la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) linapenda kuchukua nafasi hii kutambulisha rasmi Mradi mpya utakaotekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Koshuma Mtengeti alisema  mradi huwa miaka miwili utatekelezwa katika kata mbili za Wilaya ya Mpwapwa ambazo ni Pwaga na Lupeta.

Alisema lengo kuu la mradi huo ni kupunguza kuenea kwa vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto hasa watoto wa kike kwa kuhamasisha jamii kuzuia ukatili huo.

Kupitia mradi huu, shirika la CDF litafanya kazi na watoto walioko ndani ya shule, waalimu na menejimenti ya shule, viongozi wa serikali, wamiliki wa nyumba za kupanga, wahudumu wa afya, wazazi pamoja na vikundi vya kina baba ambavyo CDF inafanya navyo kazi katika kata hizi mbili,” alisema Mtengeti.

Mtengeti aliongeza kuwa ili kufikia malengo ya Mradi huo, CDF itafanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuwajengea uwezo watoto kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi na namna ya kuzuia ukatili wa kingono, kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waweze kutoa huduma bora na rafiki za afya ya uzazi kwa vijana balehe, kuwajengea uwezo wazazi, wamiliki wa nyumba za kupanga zilizo karibu na maeneo ya shule na walimu juu ya kulinda na kuzuia ukatili wa kingono kwa watoto, kuibua changamoto mbalimbali za ukatili wa kingono kwenye jamii, na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili kwa watoto kwa kutumia midahalo, vipeperushi, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.

Aidha, Mtengeti alisema shirika hilo litashirikiana na watumishi mbalimbali wa Serikali katika Halmashauri ya Mpwapwa waliopo katika ofisi ya Ustawi wa Jamii, idara ya Maendeleo ya Jamii, idara ya elimu, ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Dawati la Polisi la jinsia na watoto, Mahakama ya Wilaya, watendaji Kata na Vijiji kutoka kata za Lupeta na Pwaga pamoja na wadau wote wa ulinzi wa mtoto waliopo katika Wilaya ya Mpwapwa.

Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ni shirika la hiari lisilo la kiserikali, lililosajiliwa mwaka 2006 chini ya sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali namba 24/2002. Makao makuu ya shirika la CDF yapo mkoani Dar es Salaam na ofisi nyingine katika Wilaya za Tarime mkoani Mara na Mpwapwa mkoani Dodoma. Lengo kuu la shirika la CDF ni kutekeleza programu na mipango mbalimbali yenye kukuza, kutetea na kuboresha haki na ustawi wa mtoto wa KitanzaniaWadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo.Mratibu wa mradi huo, Asha Ramadhani akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mradi huo.

Post a Comment

0 Comments