...................................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limetoa msaada wa
futari kwa ajili ya waislamu waliofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Machi 28, 2024 kwa niaba ya
Mkurugenzi wa shirika hilo nchini na Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida,
Juma Omari alisema kila mwaka wamekuwa wakitoa msaada huo kwa waislamu ambao
wamekuwa kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu baada ya kuombwa na Sheikh wa Mkoa wa
Singida kufanya hivyo.
"Tumekuwa tukitoa chakula kwa ajli ya kuwasaidia wenzetu waislamu
ambao wanakuwa kwenye mfungo kama tulivyoombwa na Sheikh wetu wa Mkoa Issa
Nassoro, Mashirika ya Umma na Taasisi
zingine za Serikali kujitokea kuwasaidia waislamu na wale wasiojiweza katika
kipindi hiki cha mfungo ambapo wanatimiza moja ya nguzo muhimu ya dini
hiyo," alisema Omari.
Omari alisema wametoa msaada huo ikiwa ni moja ya njia ya kuwakumbuka
wananchi wa Mkoa wa Singida ambao ni wateja wao wakubwa wa matumizi ya umeme.
Alisema kutoa msaada kwa watu wasiojiweza, yatima na walio katika makundi
maalumu lipo katika miongozo ya kidini na ndio maana wamekuwa wakilitekeleza kila
mwaka.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro akipokea msaada huo alimshuruku
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida pamoja na
watumishi wote kwa kujali kwa futari hiyo walioitoa kwa ajili ya waislamu na
watu wasiojiweza.
"Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Singida
tunawashukuru sana viongozi wa shirika hili la Tanesco kwa kuwathamini na
kujali hali za wateja wao na watanzania
waliopo mkoani hapa pamoja na watu wenye mahitaj maalumu, yatima na wajane
hakika mmeonesha upendo mkubwa Mwenyezi
Mungu awape afya na maisha marefu," alisema Sheikh Nassoro.
Sheikh Nassoro alitumia nafasi hiyo kuziomba taasisi nyingine za umma na mashirika mbalimbali nazio ziige mfano wa shirika hilo kwa ajili ya kutoa msaada wa namna hiyo.
0 Comments