Amesema kuwa ongezeko la ndege na
huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na
mataifa mengine kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya
watalii wanaokuja nchini.
Amesema hayo leo (Jumanne, Machi
26, 2024) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya
ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius
Nyerere Dar es Salaam.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa ili kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae
mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege
hususan katika eneo la matengenezo na urubani.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa
amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na
kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti
upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.
Pia, Amewataka viongozi na
watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa
kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege.
Amesema kuwa usafiri wa anga
umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara.
“Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao
ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania”
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa
Majaliwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita
imesaini mikataba ya miradi mipya 6 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 674.3
inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa
Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine
yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa
Victoria.
Kwa upande wake, Waziri wa
Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa sambamba na ununuaji wa ndege za
abiria na moja ya mizigo, Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya
Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi
ya marubani kwenye soko la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.
“Pia NIT imewezesshwa mitambo na
vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya shahada na Stashahada ya
uhandisi wa ndege ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia
kwenye soko la ajira”
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi amemshukuru Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa
huduma kwa kuinunulia ndege mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika
biashara ya anga.
“Hadi sasa Serikali imewekeza
shilingi trilioni 2.4 katika ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya
kibiashara pamoja na ulipaji wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa”
Ameongeza kuwa ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27 ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano yaani 2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20 “Hadi sasa ATCL inandege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji”
0 Comments