Afisa Usalama wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Davis Mkwiche , akizungumza na waandishi wa habari (hawapo picha) kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakam ya Wilaya ya Manyoni dhidi ya Peter Yona kwa kosa la kuharibu miundombinu ya shirika hilo.
............................
Na Michael Mrisho, Manyoni
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya
Manyoni mkoani Singida imemuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela, Peter Yona
(35) ambaye ni Mkulima na Mkristo Mkazi wa Kijiji cha Igwamadete wilayani humo na kulipa faini ya Sh. 722,900 baada ya
kupatikana na kosa la uhujumu uchumi kwa kuharibu miundombinu inayotoa huduma
za kijamii mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Nassoro Saidi akizungumza na
waandishi wa habari alisema Agosti 16,
2023 majira ya jioni maeneo ya Kijiji cha Igwamadete Kata ya Iseke Tarafa ya
Heka Wilaya ya Manyoni mtuhumiwa huyo alipanda kwenye transfoma ya umeme mali
ya TANESCO na kukata waya wa ethi uliokuwa na urefu wa mita 9 wenye thamani ya
Sh.722,900 kwa kutumia sime ambapo alikamatwa siku hiyo hiyo na kufikishwa
mahakamani Septemba 5, 2023 kwa kosa hilo.
Alisema sheria kifungu namba (326) (6A) na (6B) a ya sheria kanuni ya
adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ikisomeka pamoja na paragrafu
20 (1) na 3 (a) ya jedwari namba 1 na kifungo 57 (1) na 60 (2) ya sheria ya
uhujumu uchumi na makosa ya kupanga sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022
ili mtaka mtuhumiwa kulipa hasara aliyoifanya ya Sh.722,900.
Alisema hukumu hiyo ilisomwa Aprili 5, 2024 mbele ya Hakimu Simon Kayinga
na Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Nassoro Saidi.
Akizungumzia hukumu hiyo Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Singida, Davis Mkwiche aliishukuru na kuipongeza mahakama kwa kutenda haki.
Alisema kuwa vitendo vya hujuma kwenye miundombinu ya umeme vinalitia hasara kubwa shirika ambalo linatumia fedha nyingi kurekebisha miundombinu inayoathiriwa, vinawakosesha huduma wananchi wanaohudumiwa na miundombinu hiyo na pia inaikosesha TANESCO mapato.
Alisema kwa ujumla vitendo hivyo vinarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo kwani fedha zinazotumika kukarabati miundombinu hiyo inayohujumiwa zingeweza kuongeza mtandao wa huduma kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Mkwiche alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kuhujumu miundombinu kuwa waache mara moja kwani shirika limejipanga kupambana nao na hakuna atakaye jihusisha na vitendo hivyo atakayebaki salama.
Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko aliyoyatoa hivi karibuni wakati akiliagiza shirika hilokukabiliana na vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme kwa nguvu zote wakati huu ambao uzalishaji umeme umeimarika na kuwa vitendo vya namna hiyo vinasababisha umeme kukatika na kusababisha wananchi kukosa huduma hiyo muhimu kwa tamaa ya watu wachache wanaolenga kujipatia kipato kwa njia zisizo halali.
Aidha, Mkwiche amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa kukabiliana na vitendo hivyo kwa kutoa taarifa ambazo zimekuwa ni nyenzo muhimu katika kufanikisha mapambano dhidi ya vitendo vya hujuma kwenye miundombinu na wakati mwingine wao wenyewe kuwakamata wahalifu hao.
0 Comments