Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi, akizungumza na Makatibu wa vyama vya siasa ngazi ya kata kutoka vyama mbalimbali vya siasa wanaoshiriki mafunzo ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, yalioandaliwa na TGNP, jijini Dar es salaam.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na Deogratius Koyanga, Dar es salaam
MAKATIBU wa Vyama vya siasa nchini wametakiwa kutokuwalazimisha wanawake wanaotarajia kugombea uongozi wa serikali za Mitaa kuchukua fomu za ujumbe wa Viti maalum, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanagombea nafasi za uenyekiti wa mitaa au vijiji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi, alipokuwa akizungumza na Makatibu wa vyama vya siasa ngazi ya kata kutoka vyama mbalimbali vya siasa wanaoshiriki mafunzo ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TGNP, jijini Dar es salaam.
“ ….Tumewaita nyie makatibu wa vyama ngazi ya kata kwa sababu mna jukumu kubwa sana ndani ya vyama vyenu kwa mwaka huu wa uchaguzi, tuna Imani na nyie kwamba, mkiamua wanawake wajitokeze wengi kugombea na kuteuliwa na vyama inawezekana. Tunaomba sana mkawape wanawake nafasi, muwatie moyo, wanapokuja kuchukua fomu msiwasukume kwenye viti maalum, wapeni nafasi waende kwenye viti vya kundi la wajumbe mchanganyiko, wagombee pia uenyekiti wa mitaa na vijiji”, amesema Lilian.
Aidha Lilian amesema kwamba, sambamba na suala la uchaguzi Mkuu, makatibu wa vyama ngazi ya kata wanatakiwa kuhakikisha wananchi ambao wapo kwenye maeneo yao wanashiriki kutoa maoni kwenye dira ya Taifa 2050 ili waweze kutoa maoni ya mwelekeo wa taifa kwa miaka 25 ijayo, ili pia iweze kuzingatia haki na usawa wa Kijinsia katika masuala yote ya maendeleo.
Kwa upande mwingine Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu ambaye alialikwa kushirikisha uzoefu wake wa uongozi na umuhimu wa wanawake kuwa viongozi, amesema Makatibu wa vyama wanatakiwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kwenye vyama vyao kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye shughuli za kisiasa ikiwa ni pamoja na kuondoa dhana potofu kuhusu uwezo wa wanawake.
“Makatibu mnatakiwa kuthibiti dhana potofu kuhusu wanawake viongozi, mnatakiwa kusimamia haki, kuzuia rushwa ndani ya chaguzi za chama, angalieni watu wanaotaka uongozi ambao mmewateua, wanawake wapo wangapi? Wapo wapi? Kwanini hawapo? Jiulize, kama wanakimbia uongozi ni kwa sababu gani? Chukueni hatua kuhakikisha kuna ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi” ,amesema Semu.
Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAWACHA) Sharifa Suleiman, amesema, ni muhimu wanawake wakapata nafasi katika kipindi hiki ambacho jamii imesha amaka na kutambua uwezo wa wanawake.
“Kuna mabadiliko makubwa ya kimtazamo sasa kulinganisha na miaka 15 iliyopita. Mfano kwa Zanzibar hali ya ushiriki wa wanawake ilikuwa chini sana, sasa wameanza kujitokeza, tuna Imani mwaka huu wataongezeka”, amesema Sharifa.
Taarifa ya Tume ya Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2020, inaonesha kwamba Madiwani wanawake wa kuchaguliwa kutoka kwenye kata ni 260 kati ya madiwani 3,953, sawa na asilimiua 6.58 ya madiwani wote.
Madiwani wa viti maalum ni 1,374 kwa Halmashauri zote 184, sawa na asilimia 24.59 ya madiwani wote
Kwa ujumla, madiwani wote wanawake kwenye Halmasahuri zote 184 ni 1,634 sawa na asilimia 29.24 ya madiwani wote.
Kwa mujibu wa ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka 2019, kutoka Ofisi ya Rais- Tamisemi, Kwa upande wa vijiji kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji wanawake walishinda nafasi 246 tu ambazo ni sawa na asilimia 2.1 ya wenyeviti wote, huku wanaume wakiwa ni asilimia 97.9. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa Mitaa , wanawake walishinda nafasi 528, ambazo ni sawa na asilimia 12.6, wanaume wakiwa ni asilimia 87.4 ya wenyeviti wote wa serikali za Mitaa. Kati ya nafasi 62,612 za wenyeviti wa Vitongoji wanawake walishinda nafasi 4,171, ambazo ni sawa na asilimia 6.7 ya wenyeviti wote wa vitongoji.
0 Comments