( 0754-362990 )
MJUMBE wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dkt. Zakia
Abubakar amewataka Maafisa Uandikishaji Ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi,
Maafisa Ugavi na Maafisa Teknolojia ya Habari (TEHAMA) wa Halmashauri Mkoa wa
Singida kuyapa kipaumbele makundi maalumu kama vile wazee, walemavu, wajawazito
na watoto wadogo wakati wa zoezi la kuwaandikisha wapiga kura.
Dkt. Abubakar ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo wakati
akifunga mafunzo kwa watendaji hao ngazi ya mkoa yaliyohusu uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza Septemba 14, 2024 na kufikia tamati
Septemba 15, 2024 katika Ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya
Singida.
Pia amewataka maafisa hao kuwepo vituoni muda wote hata kama
hakutakuwa na waombaji ambao watajitokeza kuomba kujiandisha.
Dkt. Abubakar aliwaambia maafisa hao kuwa mafunzo hayo
waliyoyapata yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa nadharia na vitendo kwa yale yote waliyofundishwa na kuwa wanapaswa kutekeleza majukumu waliyopewa kwa
kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na
kanuni zilizotungwa chini ya vipengere vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura.
“Napenda kutoa wito kwenu nyote kuendelea kutoa muda wenu wa ziada
kusoma na kupitia maelekezo yote mliyopewa ili kuongeza uelewa kuhusu wajibu na
majukumu yenu ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema
Abubakar.
Aidha, Dkt. Abubakar aliwaambia maafisa hao kuwa wakumbuke kwamba
maelekezo yote waliyopewa ni zana za kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa
ufanisi na kuwa wanahimizwa kuwahamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze
kujiandisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kuwachagua viongozi
wao.
.Alisema matarajio ya Tume ni kuwa mara baada ya zoezi hilo
kukamilika watu watakao kuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali.
“Jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja ninyi watendaji
kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yenu na kupitia nyenzo
mlizonazo nasisitiza mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze
mapema katika kata zote zilizopo kwenye halmashauri zenu na kazi yenu kubwa ni
kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji kwenye maeneo yenu,” alisema
Dkt. Abubakar.
Dkt. Abubakar aliwataka maafisa hao kusoma kwa makini Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo na
miongozo yote inayotolewa na Tume ili kazi yao ifanyike kwa udhanifu na haki na
wasisite kuwasiliana na Tume kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yoyote yanayohusiana
na utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) imetekeleza majukumu yake
katika hatua ya mafunzo na wao wanawajibu wa kuhakikisha wanayatekeleza yote
kwa maendeleo ya nchi.
Dkt. Abubakar alitoa wito kwa maafisa hao kufuatilia kwa karibu
zoezi hilo na kushiriki kikamilifu na kuhakikisha linafanikiwa na kuwa makini
katika eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa na muda sahihi wa ufunguaji na
ufungaji wa vituo vya kuwaandikishia wapiga kura na vilevile kuwasisitiza
watendaji waliochini yao kutumia lugha nzuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mafunzo hayo ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora alisema sasa
wapo tayari kwenda kuyafanya kwa ujuzi na weledi mkubwa yale yote waliyojifunza.
“ Tunaihadi Tume tunaenda kushiriki zoezi hili kwa uadilifu wa hali ya juu tukifahamu kwamba tumetakwa kulifanya pasi kutoa siri, sisi sasa ni sehemu ya Tume na tutakuwa makini kwa kutunza siri hadi hapo Tume itakapoona inafaa kutoa taarifa hiyo,” alisema Matomora.Mwenyekiti wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora, akitoa neno la shukurani baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo
0 Comments