...................................................
Imeandaliwa na Dotto Mwaibale / Solomoni Philemon ( 0754-362990 )
ZOEZI la uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura ambalo linafanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) sasa
ni zamu ya Mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma.
Akifungua mkutano wa Tume na wadau wa
uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Singida
Septemba 13, 2024, Mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama Kuu ya
Rufaa, Asina Omari alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na mabadiliko ya
teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi la uboreshaji wa daftari hilo.
“Tume imeboresha mfumo wa uandikishaji
ambao kwa mara ya kwanza utawezesha mpiga kura aliyepo kwenye daftari kuanzisha
mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina zote za
simu au kompyuta,” alisema Omari.
Jaji Omari alisema ni kosa la kisheria
kwa mtu yeyote kuomba kujiandisha zaidi ya mara moja atakuwa anatenda kosa
kisheria ambapo akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiopungua Sh.100,000 na
isiyozidi 300,000 au kutumikia kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi
miaka miwili au vyote kwa pamoja.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani akitoa mada
kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura alisema kwa kuzingatia
matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura 5,586,433
wapya wanatarajiwa kuandikishwa ambao ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura
29,754,699 waliopo kwenye Daftari baada ya uboreshwaji uliofanyika 2019/ 2020.
Alisema wapiga kura 4,369,531 inatarajiwa
wataboresha taarifa zao na wapiga 594,494 inatarajiwa wataondolewa kwenye
Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari hilo.
“
Kwa Mkoa wa Singida Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 216,947 hii
ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ya wapiga kura 848,456 waliopo kwenye Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema Ramadhani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Daftari na
Teknolojia ya Habari (TEHAMA), Stanslaus Mwita alisema katika zoezi la
Uboreshaji wa Daftari hilo lililoanza Julai 20, 2024 inatumika mifumo ya aina
mbili mfumo mkuu ukiwa ni VRS na mfumo saidizi ukiwa ni OVRS.
Alisema mfumo wa VRS umekuwa ukitumika
katika mazoezi ya uboreshaji yote yaliyotangulia (2015 na 2020) na kuwa mfumo
wa OVRS ulianzishwa kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa
njia ya mtandao.
Mwita alisema kwa kutumia Mfumo wa OVRS mpiga kura ili apate
taarifa zake anaweza kutumia simu janja, vishikwambi na kompyuta na watahitaji
kuwa na mtandao wa internet ili kupata
huduma hiyo ambapo wataingia katika tovuti https://ovrs.inec.go.tz
hivyo kupitia anuani hiyo waombaji wataweza kurekebisha taarifa zao, kuhama
kituo au kufanya vyote kwa pamoja.
Kwa Mfumo wa VRS unachukua taarifa za
miaka ya nyuma kama zilivyo katika fomu za uandikishaji fomu namba 1, 5A,5B na
kuwaTaarifa hizo zinahusisha, Taarifa Binafsi za mwombaji, Taarifa za Anuani za
makazi na Taarifa za Makazi ya Kudumu na nyingine zote na kuwa Mfumo wa VRS
zitatumika Alama za vidole, picha na saini.
Aidha, Mwita alisema Menu Kuu ya kupata
taarifa hizo mpiga Kura anatakiwa kupiga *152*00# na kuwa baada ya hapo atabonyeza namba 8, 2
na 3 na namba nne hapo ataweza kupata taarifa zake.
Akifunga mkutano huo Mjumbe wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Dkt. Zakia Abubakar, alisema hamasa kubwa ya
wananchi kushiriki zoezi la uboreshaji wa Daftari na baadae Uchaguzi
litachangiwa na ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwao kwa kuwafikishia ujumbe huo wananchi.
Dkt. Abubakar alitoa rai kwa washiriki wa
mkutano huo kuwaelimisha wanananchi wajue kwamba kujiandikisha au kuboresha
taarifa ndio njia pekee itakayowawezesha kushiriki kuwa chagua viongozi
wanaowapenda utakapofika wakati wa uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha
washiriki wa mkutano huo kuwa Kaulimbiu ya Uboreshaji wa Daftari hilo kuwa ni “
Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilianza
zoezi la uboreshaji wa Daftari hilo baada ya uzinduzi uliofanyika mkoani Kigoma
Julai 20, 2024 ambapo mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ulifanyika mikoa mitatu
ya Kigoma, Tabora na Katavi.
Mzunguko wa pili ulijumuisha mikoa ya
Geita na Kagera na mzunguko wa tatu ukiwa ni mikoa ya Mwanza na Shinyanga, mzunguko wan ne kwenye
mikoa ya Mara, Simiyu na Manyara katika Halmshauri ya Wilaya ya Babati,
Hanang’, Mbulu na Mji wa Babati.
Aidha, mzunguko wa tano wa uboreshaji wa Daftari hilo utajumuisha Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma, Halmashauri za Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa na Mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjirona uboreshaji utaanza Septemba 25, 2024 hadi Oktoba 1, 2024 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 na kufungwa saa 12:00 jioni.
0 Comments