*Asema watafutiwa leseni, kutaifishwa mali zao na kutoruhusiwa tena kufanya biashara nchini.
*Atoa salamu za pole kwa waarithirika wa ajali ya jengo Kariakoo
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akifurahia jambo na Viongozi na Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) baada ya kufungua mkutano wa kamati hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Karemjee, Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Rais wa FEMATA, John Bina.
...................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali haitosita
kuwachukulia hatua kali Wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini ambao
hawatafuata Sheria ya Madini na kujiingiza kwenye utoroshaji wa madini, ikiwa
ni pamoja na kuwafutia leseni, kutaifisha mali zao na kutoruhusiwa kufanya tena
biashara ya madini hapa nchini.
Amesema hayo leo Novemba 16, wakati akifungua Mkutano wa Viongozi na Kamati
Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania
(FEMATA) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Karemjee, Jijini Dar es
Salaam.
Dkt. Kiruswa amesema kupitia uongozi mpya wa FEMATA, Serikali inatamani
kuona kasoro ya utoroshaji wa madini kwa wachimbaji wadogo inakwisha sambamba
na kuelimisha umuhimu wa ulipaji kodi kwa wachimbaji wadogo wanaowaongoza ili
Serikali iweze kutekeleza ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii
ambayo inatagemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya ndani kutokana na shughuli
mbalimbali za uchumi ikiwa ni pamoja na shughuli za madini.
“Wizara isingependa kuona uwepo wa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara
ambao siyo waaminifu, Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali wachimbaji
wote na wafanyabiashara wa madini ambao hawatafuata Sheria ya Madini ikiwa ni
pamoja na kuwafutia leseni na kutaifisha mali zao” amesema Dkt. Kiruswa.
Ameeleza kuwa, mikakati iliyopo kwa Serikali ni pamoja na kuwapatia
Wachimbaji Wadogo maeneo ya uchimbaji na kusaidia kufanya utafiti kwa bei ndogo
yenye ruzuku ya Serikali kupitia Shirika letu la Madini Taifa (STAMICO).
“Nitoe rai kwa Wachimbaji Wadogo nchini kuchangamkia fursa hiyo ya
kufanyiwa utafiti wa uchorongaji na STAMICO kwa bei nafuu yenye ruzuku ya
Serikali” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Vilevile, Dkt. Kiruswa amewataka kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii
kujenga na sio kulumbana na kujadiliana mambo ya msingi kwa kuwa shirikisho
hilo ni la kibiashara na kwamba matarajio ya serikali ni kuona FEMATA inapiga
hatua kubwa huku wanachama wakizika tofauti zao.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa kwa niaba ya Viongozi na watumishi wa
Wizara ya Madini, ametoa pole kwa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Ofisi ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa ajali
iliyotokea jana tarehe 16 Novemba 2024, ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne
katika Mtaa wa Congo na Mchikichi, Kariakoo Jijini Dar es salaam huku
akipongeza juhudi za uokozi zinazoendelea na kuwaombea kukamilisha zoezi hilo
salama na kuwaokoa ndugu zetu wakiwa salama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahaya Samamba
ameipongeza FEMATA kwa mabadiliko chanya yaliyoleta utulivu katika Sekta ya
Uchimbaji Mdogo na kuainisha kuwa Serikali kupitia Wizara inaunga mkono juhudi
za FEMATA na wachimbaji wadogo kwa ujumla.
Sambamba na hilo, Mhandisi Samamba ameilekeza FEMATA kufanya marekebisho ya
Katiba ya Shirikisho hilo, kwa kuwa itasawaidia kugawa majukumu, kuanisha maono
na mipango yao kwa maendeleo endelevu.
Amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi
yote ya wachimbaji ili kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa tija ikiwa ni
pamoja na kkuwapatia maeneo ya kuchimba pamoja na kuratibu mikopo nafuu
kufuatia majadiliano mazuri na taasisi za kifedha na mabenki.
Naye, Rais wa FEMATA John Bina amesema kuwa Mkutano huo wa FEMATA umelenga
la kuwasaidia viongozi wa shirikisho hilo ili waweze kutimiza wajibu wao kwa
ufanisi zaidi na hatimaye kuleta matokeo chanya huku akimhakikishia Naibu
Waziri Dkt. Kiruswa kuwa Shirikisho hilo litaendelea na kutoa elimu kwa
wachimbaji wadogo kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kutumia masoko na vituo vya
ununuzi vya madini kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Vilevile, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira
mazuri ya uwekezaji hapa nchini ikiwa ni pamoja na mazingira bora kwa
wachimbaji wadogo.
Rais wa FEMATA, John Bina.akiwa kwenye mkutano huo.
Wadau wa uchimbaji wakiwa kwenye mkutano huo.
0 Comments