................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa
vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuwa vinara katika
kulinda amani na kukemea viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.
“Hamasisheni wanachama wenu kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia
kudumisha amani iliyopo. Wananchi wote waliojiandikisha katika orodha ya
wapigakura wa Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wajitokeze kwa wingi
kupiga kura katika vituo vyao siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024. Siku
hiyo itakuwa ya mapumziko maalum kwa ajili ya uchaguzi huo.”
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Novemba 10, 2024) wakati alipomwakilisha
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu na Kongamano la
Umuhimu wa Amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amewasihi Watanzania na viongozi wa dini kuendelea
kuitangaza amani ndani na nje.”
Katika Kongamano hilo, ambalo linaratibiwa na Jumuiya ya Waislamu wa
madhehebu ya Shia Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo
kuwasisitiza viongozi hao kuhamasisha wanachama wao kushiriki katika uchaguzi
huo huku wakizingatia suala la kudumisha amani kwa muhimu mkubwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ajitokeze
kupiga kura ili kuwachagua vongozi ambao
ni mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe
wa serikali za vijiji na kamati za mitaa. “Ikumbukwe kuwa kupiga kura ni wajibu
na haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania.”
Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na
kuthamini kazi kubwa inayofanywa na madhehebu ya dini pamoja na taasisi zote,
ambapo licha ya kutoa mafundisho ya kiroho, taasisi za dini zimekuwa zikiunga
mkono jitihada mbalimbali za Serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa
wananchi.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Alhad Mussa Salum ameipongeza Jumuiya ya Waislam wa Shia Tanzania kwa harakati zake za kuhakikisha amani na utulivu wa Tanzania unaendelea kukua. Mimi ni shuhuda mzuri wa harakati za Shia wanazofanya ili kuhakikisha amani na usalama wa Tanzania unaendelea kuimarika.
0 Comments