.....................................
Na Ashrack Miraji, Tanga
Zaidi ya asilimia 85 ya maandalizi ya tukio la Magamba Forest Walkathon and Adventure Season III yamekamilika, huku waandaaji wakieleza kuwa kila kitu kinaendelea vizuri kuelekea kilele cha tukio hilo. Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 20 Desemba katika Manispaa ya Lushoto, mkoani Tanga.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Misitu ya Mazingira Asilia Magamba, Christoganus Vyokuta, amesema kuwa kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba, wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii watapata fursa ya kujitangaza na kuonesha huduma na bidhaa zao mjini Lushoto.
Vyokuta amesema kuwa kilele cha tukio hilo kitafanyika tarehe 20 Desemba, ambapo washiriki watahusika katika matembezi maalumu ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Magamba, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani na uhifadhi wa mazingira.
Ameeleza kuwa lengo kuu la Magamba Forest Walkathon and Adventure Season III ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika suala zima la uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii ikolojia, hususan kwa kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini.
Mhifadhi huyo amewataka wananchi na wadau wa sekta ya utalii kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kulinda rasilimali za asili na kuhakikisha uhifadhi endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



0 Comments