Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akizungumza na timu ya Tanzania Broweries Ltd. (hawamo pichani) wakati alipotembelea kiwanda chao jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa
Sera Bw. Elijah Mwandumbya asikiliza majadiliano kati ya Timu ya Wizara ya
Fedha na Timu Tanzania Breweries Ltd (hawamo pichani) yaliyofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha bia chaTBL jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa
Madeni Bw. Japhet Justine asikiliza majadiliano kati ya Timu ya Wizara ya Fedha
na Timu Serengeti Breweries Ltd (hawamo pichani) yaliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa kiwanda cha bia cha Serengeti Breweries jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akiwa kwenye majadiliano na timu ya kiwanda cha bia cha Tanzania Breweries Ltd (TBL) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni timu ya Wizara ya Fedha na Mipango na kulia ni timu ya TBL
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (kulia ) Pamoja na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango walipotembelea kiwanda cha Tanzania Breweries Ltd. (TBL) kushoto niMkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John Wanyancha (kushoto), kulia ni Kamishna wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Na Eva Ngowi,Wizara ya Fedha na Mipango
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya
Fedha na Mipango inataka kuangalia upya tozo za stempu za kielektroniki (ETS)
ambazo kwa miaka mitatu iliyopita sekta ya viwanda imekuwa ikilalamika kuwa
tozo hizi zimekuwa kubwa, hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
na Mipango Bw. Lawrence Mafuru alipokuwa katika ziara ya kutembelea viwanda vya
kutengeneza bia vyaTanzania Breweries Ltd na Serengeti Breweries Ltd jijini Dar
es Salaam.
“Kuna haja ya Serikali kusikiliza hoja hii haiwezekani kwamba kuna
kitu ambacho wenzetu wanakiona na sisi hatukioni. Kwa mrejesho ambao tumeupata
na sisi tumejionea mfumo unavyofanya kazi, lakini pia tumepata fursa ya kuona
mfumo mwingine ambao unafanya kazi sambamba na mfumo unaolalamikiwa, sasa huo mwingine
unatumia ‘block chain technology’ ni almost bure na sasa tunajiuliza nini
ambacho hatukioni; ambacho wenzetu wanakiona,”Alisema Bw. Mafuru
Bw. Mafuru alisema kuwa atawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) ili waeleze kwa kina ni nini hasa ambacho wamekibaini kwenye huo
mfumo.
“Wawekezaji hawa ambao wako tayari na hawapingi mfumo
wa stempu za kielektroniki wanausapport kabisa ila wanachokisema una gharama na
kwa hakika ukiangalia gharama zinazozungumzwa kama zingekuwa hazilipwi maana
yake ni kwamba zingekuwa sehemu ya mapato ya Serikali.” Alisema Bw. Mafuru
Bw. Mafuru alisema nia hasa ya kufanya ziara hii ni kutimiza
wajibu wa Wizara ya Fedha katika eneo la kusimamia uchumi kwani maendeleo ya
nchi pamoja na uchumi wa Tanzania unategemea sana ushiriki wa sekta binafsi
katika uzalishaji na utoaji wa ajira.
“Ziara hii imelenga kutuwezesha sisi kuelewa kwanza changamoto
ambazo wenzetu kwenye sekta hii hasa sekta ya utengenezaji wa vinywaji,
changamoto gani wanazopitia Pamoja na kupata mrejesho kutoka kwao kuhusu sera
za hivi karibuni za kibajeti ambazo tumezipitisha kupitia bajeti ya
Serikali, Sheria ya fedha lakini pia utekelezaji wa ile blue print,
ambayo Serikali imekuwa ikiendelea kutekeleza. Hivyo tunafanya jitihada
ya kupata mrejesho na hatimae tuweze kujua wapi ambapo tunahitaji kuongeza
jitihada, wapi tunafanya vizuri na wapi hatufanyi vizuri ili tuweze kurekebisha
kwa kujua kwamba tutakapoendelea kurekebisha maeneo hayo basi tutaendelea
kuifungua nchi yetu kiuchumi” Alisema Bw. Mafuru
Aidha Bw. Mafuru alisema jambo muhimu sana ambalo ameliona ni
kwamba; kuna haja Serikali kufanya kazi kwa Pamoja kwani kila mtu
akifanya kazi kwenye eneo lake peke yake atairudisha nyuma na kuiuchelewesha
Serikali.
Alisema kuwa Kuna hoja ambazo viwanda hivyo vimeziibua
ambazo zinahitaji Taasisi na Wizara zingine za kisekta ziweze kuingilia
na kufanya maamuzi kwani kuna maamuzi yako tangu mwaka 2016 ambayo yangetakiwa
kufanyika ili kwa wanaohitaji kuwekeza waweze kuwekeza. Hivyo amesema
wamechukua hili angalizo na watakaa na TRA ili kujua nini hasa hoja yao.
Bw. Mafuru aliongeza kuwa ili kuongeza uwekezaji nchini inapaswa
kuwawekea mazingira rafiki ya kuwa na uhakika kama mitaji yao iliyopo hapa
Tanzania italindwa ili waweze kuleta mitaji mingine.
“Makampuni yote mawili tuliyoyatembelea leo yana mipango ya
kuongeza uwekezaji wao nchini lakini kuna kitu kinang’ang’ania kwenye
mawazo yao ya kutokuwa na uhakika kama mambo yale ambayo yana miaka
mitatu, minne hayajashughulikiwa ni kitu gani kinawapa guarantee waje kuongeza
mitaji yao, kwa hiyo kuna hoja hapa ambayo na sisi tumepata mrejesho ambao
tutakwenda kushare na wenzetu Serikalini na Mamlaka zinazohusika kwa lengo la
kuratibu na jitihada za Serikali ili tuweze kuyashughulikia haya mambo ambayo
ni kikwazo katika ukuzaji wa hizi sekta”. Alisema Bw. Mafuru
Bw. Mafuru alisema kuhusu fursa za uwekezaji, kuna changamoto ya
upungufu kwenye soko la chupa za kujaza bia na uzalishaji huo umekuwa kwa
muda mrefu unategemea kiwanda kimoja tu hapa nchini. Kwa kuwa wametuambia
wengine wako chini ya kiwango chao cha uzalishaji na kwa sababu tu ya ukosefu
wa chupa, hii inatuambia kisera inabidi kufanyike jitihada za kuwezesha
sekta hiyo ya uzalishaji wa chupa ili kuweza kuongeza uzalishaji huu.
“Kwa hivyo ni sekta ambayo iko coordinated tukijua kwamba sasa
kuna changamoto ya chupa na tutaongea na Wenzetu wa Wizara ya Viwanda Biashara
na Uwekezaji waweze kuangalia namna gani wana fast truck wawekezaji ambao
wanaweza kuwekeza katika ilo eneo kwa sababu kuna fursa na bahati nzuri fursa
hii sio tu kwa Tanzania chupa zetu zinauzwa hadi nchi Jirani kwa hiyo
itatusaidia kupata fedha za kigeni kwa hivyo ukiona ni bia lakini inapanua na
mambo mengine ambayo ndio uchumi wenyewe. Alisema Bw. Mafuru
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia
Mwamboka alisema wana matumaini kwamba mazungumzo yaliyofanyika leo na
timu ya Wizara ya Fedha na Mipango yataleta tija kwa nchi na wako tayari kutoa
ushirikiano kwa Serikali kwa lengo la kutanua wigo wa kukusanya kodi. Pia
aliongezea kwenye suala la stempu za kielektroniki alisema kuwa ni mfumo mzuri
ambao ulianzishwa na TRA lakini bei ni kubwa japo wanaamini kuwa Serikali
inalifanyika kazi.
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw.
John Wanyancha alisema wamerafijika sana kwa ujio wa viongozi kutoka Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango kusikilia malalamiko yao na kuona jinsi ambavyo
wanafanya kazi. Wanaamini kwamba hii ziara ya Serikali kuja kuwasilikiliza
wawekezaji ni njia nzuri sana ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya
viwanda hapa Tanzania.
Katika suala la huduma za kijamii Serengeti Breweries Company Ltd.
wameweza kuzalishaji ajira za moja kwa moja katika kiwanda chao, pia jukumu la
usafirishaji linafanywa na kampuni binafsi ya Watanzania ambao wanapata kipato
chao kutokana na sekta hii ya uzalishaji bia. Pia wanatoa ufadhili kwa
wataalamu wa kilimo kwa sababu wana utaratibu wa kununua ngano ambayo
wanaitumia kutengeneza bia. Hivyo wataalamu ambao waliwasomesha ndio
wanaosaidia kutoa elimu ya kuboresha mazingira ya uzalishaji kwenye mashamba
yao.
Sekta hizi za vinywaji ndio hasa zimekuwa kinara katika uchangiaji kwenye eneo la kodi ni vyema Serikali ifanye jitihada za kutatua changamoto zao ili waendelee kuchangia kwa sehemu kubwa na waendelee kukua na kuongeza ajira, kuleta maendeleo ya kiuchumi ambayo ndiyo matarajio ya Serikali.
0 Comments