Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (katikati) akikagua ujenzi wa daraja la Mwanga linalojengwa wilayani Mkalama.
..............................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameridhishwa na utekelezwaji wa
ujenzi wa miundombinu ya barabara inayotekelezwa na Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa Singida.
Akikagua leo Februari 20, 2024 ujenzi wa miundombinu ya madaraja na makalavati katika Wilaya ya
Iramba na Mkalama, Serukamba amepongeza ubunifu na ufanisi ambao umepelekea
kufanikisha miradi hiyo kwa ustadi mkubwa.
“Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha analeta fedha za
kutosha ili kuhakikisha miundombinu ya
wana Singida inakidhi mahitaji ya ustawi wa kijamii na uchumi na masuala yote
ya kimtambuka kwa maendeleo ya nchi.
Serukamba akizungumzia ujenzi wa barabara ya Meli-Walla, Ntwike ya kilometa
23 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 669 inayojengwa Wilaya ya Iramba
alisema mara itakapokamilika itasaidia kurahisisha mawasiliano ya masoko ya
mazao na shughuli za uvuvi katika eneo hilo na kufika makao makuu ya wilaya
hiyo.
Aidha, Serukamba alimuomba Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi
Ibrahimu Kibasa na timu yake kuomba maombi maalumu Serikalini ya fedha za
ujenzi wa daraja la mto Ntwike ambalo barabara hiyo itapita kwani bila ya ujenzi wa daraja hilo ujenzi wake
hutakuwa hauna maana yoyote.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa akizungumza
katika ziara hiyo ya siku moja ya RC Serukamba alisema lengo la ujenzi wa
barabara hiyo ni kupunguza umbali wa kusafiri zaidi ya kilometa 40
kutoka Shelui hadi makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa kupitia
barabara ya kuzunguka ya Misigiri lakini kwa kutumia barabara hiyo mpya watatumia kilomita
23 tu kufika Kiomboi ambako ni makao makuu ya wilaya.
Miundombinu iliyokaguliwa na Serukamba katika ziara hiyo ni ujenzi wa
barabara ya Mwanza inayojengwa wilayani Iramba ya kilometa 1.5 na Old Kiomboi.
Serukamba kesho Februari 21 anatarajia kuendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Ikungi na Singida.
0 Comments