Na. Rahma Taratibu (SJMC)
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kujadiliana na
wafanyabiashara wenye malimbikizo ya kodi ili kuwapa unafuu wa kulipa
malimbikizo ya kodi kwa awamu bila kuathiri ukwasi, mwenendo na uendeshaji wa
biashara.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan
Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asha Abdullah
Juma kuhusu hatua zinazochukuliwa kwa
walipa kodi walioshindwa kulipa na kuwa na malimbikizo makubwa lakini wapo
tayari kulipa kutokana na agizo la Mhe. Rais.
Mhe. Chande alisema kuwa majadiliano hayo yanayoendelea na wafanyabiashara
ni katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
“Sheria ya Usimamizi wa Mapato, Sura
438 Kifungu cha 70 na Kanuni zake kinampa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kusamehe adhabu na riba kama kuna suala na sababu maalum”
alibainisha Mhe. Chande.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande
(Mb) alisema kuwa Serikali ilifuta utaratibu kwa walipakodi kulipa kodi kabla
ya kuanza biashara ili kutoa nafasi ya kujiimarisha kibiashara.
Alisema hayo alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Zainab
Athuman Katimba, aliyetaka kujua muda ambao Serikali itaondoa utaratibu wa
biashara mpya kutakiwa kulipa kodi ya mapato kabla ya biashara kuanza.
Mhe. Chande alisema mwaka 2019/20 baada ya Serikali kufuta utaratibu huo
walipakodi wote wanatakiwa kulipa kodi miezi sita (6) baada ya kufungua
biashara na kuongeza kuwa utozaji wa kodi ya mapato hufanyika kulingana na
mapato yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka husika.
Aidha, aliiagiza TRA kuendelea kufuata sheria, utaratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
0 Comments