Mchungaji Yona Ezekiel wa Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba Singida |
Na Dotto Mwaibale, Singida WAZAZI na walezi wenye watoto walio katika
makundi maalumu (walemavu) wametakiwa kutowafungia ndani badala yake wawapeleke
shuleni na kwenye vyuo vya ufundi wakapate mafunzo ya fani mbalimbali. Ombi hilo limetolewa na Mchungaji Yona Ezekiel wa
Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba,Machi 12, 2023 katika ibada iliyohudhuriwa
na Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho
kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba kilichopo Manispaa ya Singida. “Leo Mungu ametupa baraka kubwa ya
kutembelewa na watoto wetu kutoka Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye
Ulemavu Sabasaba na tumeona vipaji vyao vya uimbaji” alisema Ezekiel. Ezekiel alisema wanafunzi hao wanafundishwa
fani mbalimbali za ufundi kama umeme, uokaji wa keki, uchomeleaji, ufundi
rangi, ushonaji, masuala ya saluni, uselemara, utengenezaji wa simu na
upambaji. Alisema wapo wanafunzi ambao wamefikia hadi
masomo ya juu na kuwa wahandisi na wataalam katika maeneo mbalimbali hapa
nchini hivyo wazazi wasiwanyime watoto wao fursa ya kupata mafunzo hayo
yanayotolewa bure na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Alisema mtoto kuwa mlemavu hakumfanyi
hashindwe kufanya chochote kwani kila mmoja anaweza kujifunza fani yoyote
kulingana na ulemavu alionao na sio kuwatenga au kuwafungia ndani. Mchungaji Ezekiel akihubiri neno la Mungu
kutoka kitabu cha Yohana 4:27-42 akimuongelea mwanamke msamaria katika kisima cha Yakobo wakati Yesu Kristo
alipokuwa akitoka Uyahudi akielekea Galilaya kupitia Samaria alimshangaa
mwanamke huyo akichota maji kisima cha mbali ili hali kulikuwa na visima
jirani na eneo alilokuwa akitoka huku akichota maji hayo mchana badala ya asubuhi na
jioni muda uliokuwa umezoeleka. Baada ya mshangao huo Yesu alimuomba maji mwanamke
huyo msamaria ambaye alimwambia Wayahudi na Wasamaria hawachangamani kwa lolote na
inakuaje amuombe maji lakini Yesu alimjibu kuwa angemjua anayemuomba hayo maji
angemuomba maji ya uzima. Mwanamke huyo msamaria alimwambia Yesu kuwa
hana chombo cha kuchotea maji wala kisima na isitoshe ni kirefu hivyo
atapata wapi hayo maji ya uzima. Yesu alimwambia kila atakayekunywa maji ya
kisima cha Yakobo ataona kiu, lakini atakayekunywa maji atakayompa yeye hataona
kiu milele ndipo mwanamke huyo msamaria alipoomba apewe maji hayo ya uzima. Mchungaji Ezekiel alitolea mfano huo
akilinganisha na maisha yetu ya leo ambayo yamejaa utengano, ukabila, hakuna
umoja, upendo jambo linalosababisha maendeleo ya nchi na huduma za kiroho kurudi nyuma badala ya kusonga
mbele na kukithiri kwa vitendo vya ukatili. Mchungaji Ezekiel alitumia nafasi hiyo
kuiomba jamii kuwa na upendo, kuacha ukabila, umajimbo na badala yake kujenga
umoja wa kitaifa kwa ajili ya kuijenga nchi yetu ya Tanzania na kila mmoja kuabudu kwa imani na dini yake kwa amani na utulivu jambo litakalo mpendeza Mungu. Aidha Mchungaji Ezekiel ameendelea kuwaomba
wadau mbalimbali kusaidia ununuzi wa kiwanja cha kujenga Kanisa la Moravian
Parish ya Sabasaba kwani hivi sasa wanafanya ibada zao katika kanisa la muda
walilolijenga kwa kutumia miti na mabati. Mchungaji Ezekiel aliomba kwa mtu yeyote, Taasisi, Wafanyabiashara na madhehebu mbalimbali watakao kuwa tayari wanaweza kutoa kiasi chochote cha fedha kupitia Akaunti Namba 50810046663 Benki ya NMB Kanisa la Moravian Sabasaba Singida mjini au awasiliane na Mchungaji Yona Ezekiel kwa namba 0758148508. |
0 Comments