RC SINGIDA ATAKA WAAJIRI SEKTA BINAFSI KUTOA AJIRA KWA WALEMAVU

Subscribe Us

RC SINGIDA ATAKA WAAJIRI SEKTA BINAFSI KUTOA AJIRA KWA WALEMAVU

Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo lililofanyika Ukumbi wa Romani Katoliki Singida 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewaomba waajiri wa sekta binafsi ndani ya mkoa kutoa ajira kwa watuwenye ulemavu. 

Serukamba ametoa ombi hilo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Ali Mwendo, wakati wa Kongamano la watu wenye ulemavu mkoa hapa, lililolenga kujadili fursa mbalimbali zikiwamo za kiafya na kiuchumi. 

“Nipende kuwashukuru sana kwa risala yenu nzuri ambayo imejaa hekima na busara na namna mlivyoeleza mafanikio ya Mheshimiwa Rais wetu kwa kipindi cha miaka mwili ya uongozi wake.

“Niongeze kuwa katika mkoa wetu mambo kadhaa yamefanyika kwa kundi la watu wenye ulemavu katika sekta ya afya, elimu na miundombinu. 

“Nimezisikia na kuzipokea changamoto zenu ambazo mmeanisha kwenye risala yenu hasa suala la ajira kwa watu wenye ulemavu katika sekta binafsi.

“Niwasihi waajiri wote wa sekta binafsi ndani ya mkoa wa Singida kutimiza takwa hili la kisheria Na. 9 ya mwaka 2010 inayoelekeza kuwa kila mwajiri anapo ajiri watumishi 20 asilimia 3 wanatakiwa kuwa watu wenye Ulemavu,” alisema.

Mwendo akizungumzia kuhusu ombi la mikopo ya asilimia mbili alisema itolewe kwa Watu wenye ulemavu kwa kupatiwa bidhaa na sio fedha ili iweze kuleta tija. 

“Kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye masuala ya fursa za elimu na kiuchumi, ninyi wenyewe ni mashahidi wa namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyo wajali na kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali,” alisema Mwendo.

Alitoa mwito kwa watu wenye ulemavu wajiunge kwenye vikundi vya ujasiriamali ili kunufaika na fursa mbalimbali za kifedha hususan mikopo. 

“Niwaombe watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wetu wa Singida ili kukuza uchumi wetu na pia tuendelee kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan Mungu ampe afya njema ili azidi kutuletea maendeleo zaidi,” alisema Mwendo kwa niaba ya Serukamba.                                     

Awali Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Singida, Richard Daudi akisoma risala yao alisema wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa ofisi na ukosefu wa vitendea kazi pamoja na ukiritimba katika masuala ya ajira hususa kutoka sekta binafsi.

Hivyo ameiomba Serikali iwaunge mkono katika kuboresha mazingira ya ofisi hiyo na kutatua changamoto za kiafya na kiuchumi zinazo wakabili.




 

Post a Comment

0 Comments