Baadhi ya wanafunzi wapya wakifurahia maisha yao ya shule mara baada ya kuandikishwa (Picha kwa Hisani ya Mtandao)
Na Abby Nkungu, Singida
JUMLA ya watoto 54,710 wenye umri usiozidi miaka sita wameandikishwa
kuanza masomo ya awali kwenye shule
mbalimbali zilizopo halmashauri za mkoa wa Singida katika kipindi cha Januari
hadi Machi 10 mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya elimu.
Taarifa ya idara ya elimu iliyotolewa kwenye kikao cha Kamati ya ushauri ya
mkoa wa Singida (RCC) inaonesha kuwa idadi hiyo ya watoto walioandikishwa ni
sawa na asilimia 99 ya lengo la kuandikisha watoto 55, 262.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa kati ya walioandikishwa kuanza masomo ya
awali, 27,953 ni wavulana na 26,757 ni wasichana ambapo miongoni mwao 58 ni
watoto wenye mahitaji maalumu.
Imeelezwa kuwa Wilaya ya Ikungi ndiyo inayoongoza kwa kuandikisha watoto
12,076, ikifuatiwa na Wilaya ya Singida
watoto 11,060, Mkalama (7,919), Iramba (7,868), Manispaa ya Singida
(6,378), Manyoni (4,597) na Itigi watoto 4,812.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya
Singida, Elia Digha alisema kuwa idadi kubwa ya watoto walioandikishwa mwaka
huu inaonesha kuwa jamii imeanza kuelewa na kutambua kuwa elimu ya awali ni
muhimu katika kumuandaa mtoto kuanza darasa la kwanza.
“Ukiangalia makadirio yalikuwa kuandikisha zaidi ya watoto 55,000 lakini
tumefikia 54, 000 ni hatua nzuri kwa jamii yetu kuanza kuwa na
mwitikio mkubwa wa kuandikisha watoto
elimu ya awali” alisema na kuungwa mkono na
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega ambaye
alisema hata kiwango cha ubora wa elimu kinaweza kupanda kwa watoto kuanza
kuandaliwa mapema kimasomo kabla ya
kuanza darasa kwa kwanza.
“Ujue yanapokuja matokeo ya darasa la saba mara nyingi unakuta shule za
Mjini zinafanya vizuri zaidi kuliko za kwetu Vijijini. Hii ina maana kwamba
pamoja na miundombinu, walimu na mengine, lakini wenzetu msingi mkubwa na mzuri
unaanzia kwenye chekechea” alisema.
Alifafanua kuwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo
ya Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2021 imesadia katika
kuleta mwamko huo wa elimu ya awali.
“Programu hii inalenga watoto wa chini ya miaka 8 umri ambao ndio wa Chekechea, darasa la kwanza au
la pili, na masuala yanayoangaliwa zaidi
ni elimu, afya, lishe, ulinzi, usalama na mengine mtambuka. Kwa hiyo, naweza kusema uandikishaji huu ni
sehemu ya mafanikio ya Programu hiyo” alieleza.
Naye Hamisi Ali mkazi wa Sabasaba na
Anna Elia mkazi wa Utemini mjini Singida wanasema, pamoja na mwitikio
chanya wa wazazi na walezi kupeleka
watoto wao kuanza masomo ya awali bado kuna haja kwa Serikali kuweka mazingira
rafiki kwa kundi hilo kupata elimu.
“Wenzetu wa shule binafsi kuna kitu wanatuzidi.... wana sehemu ya michezo,
uji au chai na chakula, mazingira safi pia usafiri. Kwa hiyo, mtoto anavutiwa
kwenda shule ila sasa hizi za Serikali baadhi yake hata uji hakuna na kwa mtoto
mdogo lishe ni muhimu kumjenga kiakili” anasema
Hamisi na kuungwa mkono na Anna ambaye anataka shule za awali ziboreshwe
zaidi kuvutia watoto wadogo.
Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuifanya elimu ya Awali kuwa ya lazima kwenye Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kuijumuisha elimu ya Awali katika elimu za Msingi kwa kuzitaka shule zote kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto wa chini ya miaka mitano.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega akichangia jambo katika moja ya mkutano mkoani hapa hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha akizungumza katika moja ya kikao mkoani hapa hivi karibuni.
0 Comments