Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa
Singida limeendesha bonanza maalumu la michezo ya aina tofauti tofauti na kuwashirikisha watumishi wa kada
mbalimbali wakiwemo kutoka idara ya uhasibu, ufundi, madereva, idara ya dharura
ambao walitoka katika wilaya zote mkoani hapa.
Akifungua bonanza hilo lililofanyika katika
Uwanja wa Peoples mjini hapa Meneja wa
shirika hilo Mkoa wa Singida Mhandisi Florence Mwakasege aliwapongeza watendaji
wote wa shirika hilo kwa kutoa ushirikiano na kufanikisha bonanza hilo.
“Kwanza niwapongeze watumishi wote mliosafiri na
kuja kushiriki bonanza hili ambalo ni la
muhimu sana kwetu kwani ni sehemu ya mazoezi ambayo ni afya nawapongezeni kwa
kuja na kuifanya siku hii kuwa ni ya
pekee na yenye furaha kwa kila moja
wetu," alisema Mwakasege.
Aidha, Mhandisi Mwakasege alisema michezo ni
upendo, amani na mshikamano na kuwa wanapokutana kwenye michezo wanaunganisha
umoja wao na kuimarisha afya zao.
"Kamati ya maandalizi imejipanga vizuri na
kila mmoja atashiriki mchezo wowote atakaoutaka kwani michezo yote ni yetu,
siku ni yetu shughuli ni ya kwetu na watu ndio sisi hakuna Tanesco nyingine
zaidi ya hii," alisema Mwakasege.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja wa shirika
hilo Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo alisema pamoja na bonanza hilo kuwa la
michezo pia lengo kubwa ilikuwa ni kutoa ujumbe kwa jamii kuacha kupanda miti
chini ya miundombinu ya umeme na kuhamasisha matumizi ya namba ya huduma kwa
wateja inayopokea taarifa kutoka kwa wateja wao wanaotumia nishati hiyo ambayo
ni 0748-550000.
Mwaipopo alisema bonanza hilo lilihusisha michezo
ya kukimbiza kuku, kuvuta kamba, mpira
wa miguu uliochezwa na timu ya Tanesco na Singida Veterans, mchezo maalumu wa
aina yake wa kunywa soda na mkate,kushindana
kula tunda aina ya Aple huku mikono ikiwa imewekwa nyuma, kukimbiza
kuku, kuvuta kamba, kutembea na yai likiwa kwenye kijiko na mazoezi ya viungo.
Katika
shindano la kukimbiza kuku aliyeibuka mshindi ni Christopher Wando shabiki wa
timu ya Singida Veterans aliibuka mshindi kwa
upande wa wanaume na kwa wanawake akiwa ni Rose Abdallah huku mshindi wa
unywaji wa soda aina ya cocacola akiwa
ni Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Utemini, Aisha Miraji.
Mshindi wa kunywa soda na mkate alikuwa ni
mfanyakazi wa Tanesco Yohana Wambura, huku mshindi wa kula tunda aina ya Aple
akiwa ni Asiatu Mnanura kwa upande wa wanawake na kwa upande wa wanaume akiwa
ni Selemani Mwanga.
Mshindi wa kutembea huku yai likiwa limewekwa
kwenye kijiko kikiwa mdomoni akiwa ni Mfanyakazi wa Tanesco, Nassoro Mangi kwa
upande wa wanaume na kwa upande wa wanawake akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Utemini, Diana
Thomas.
Katika mchezo wa kuvuta kamba wafanyakazi wa
Tanesco waliibuka kidedea dhidi ya Singida Veterans.
Baada ya michezo hiyo iliyonza saa tatu asubuhi
hadi saa 8 mchana watumishi wote wa Tanesco ambao walikuwa ni wenyeji
walijumuika na wageni waalikwa katika
hafla “Get Together Party’’ iliyofanyika
katika Ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA kwa lengo la kupongezena na kuondoa
uchovu, sanjari na kuwaaga wafanyakazi watatu wa shirika hilo waliostaafu ambao
ni Juma Mafula, Andendekisye Mwakipesile na Msikai Mwankoo na wafanyakazi tisa waliohamishiwa vituo vingine vya kazi
akiwepo aliyekuwa Meneja wa Tanesco Singida ambaye amehamishiwa makao makuu
kuwa Meneja wa Kitengo cha Wateja wakubwa, Mhandisi Francis Kaggi.
Katika sherehe hizo mgeni rasmi alikuwa ni Mkurugenzi wa Kanda ya Kati, Mhandisi Frank Chambua.
0 Comments