Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akiwakabidhi viongozi wa Kata ya Misughaa mifuko ya saruji 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 8 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hosteli ya Shule ya Sekondari ya Dk. Ali Mohammed Shein iliyopo Kata ya Misughaa wilayani Ikungi Mkoa wa Singida katika hafla iliyofanyika jana May 8, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ametoa mifuko ya
saruji 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 8 kwa ajili ya kusaidia ujenzi
wa hosteli ya Shule ya Sekondari ya Dk.Ali Mohammed Shein iliyopo Kata ya Misughaa wilayani
Ikungi Mkoa wa Singida.
Mbali ya kukabidhi saruji hiyo pia ametoa kompyuta nne pamoja na Projekta moja ili iweze kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo ambayo ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kimasomo wilayani humo.
Akizungumza wakati akikabidhi saruji hiyo Mtaturu alisema ni utekelezaji wa
ahadi yake aliyoahidi ili kuanza ujenzi wa hosteli hiyo haraka iwekanavyo kwa
ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo hasa wa kike kuwapunguzia kutembea
umbali mrefu kufika shuleni.
"Leo hii nimeleta saruji mifuko 100 kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi na
mifuko yote 400 nimekwisha ilipia na lengo langu nataka tuanze haraka kufanya mchakato
wa ujenzi ikiwa ni utekelezaji wa ilani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mtaturu alisema imeletwa mifuko hiyo 100 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo huku
akihofia ikipelekwa inaweza kuharibika na kuwa hasara kwani jambo hilo
siku za nyuma kabla ya kuwa mbunge lilikwisha tokea katika moja ya kata ambapo
mifuko zaidi ya 60 iliganda kutokana na kuchelewa kuitumia.
Mbunge Mtaturu alisema kazi hiyo inafanyika ikiwa ni kumuunga mkono Rais
Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ya shule ili watoto wasome
katika mazingira bora chini ya kauli mbiu ya Serikali ya kutoa elimu bure kuanzia
shule ya msingi hadi sekondari.
"Rais wetu Samia amefanya kazi kubwa ya kutoa fedha nyingi katika nchi
yetu kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi ya maendeleo na jimbo letu la Singida
Mashariki likiwa ni mnufaika ya fedha hizo hivyo sisi tukiwa ni wawakilishi wa
wananchi tunakila sababu ya kumuunga
mkono kwa kumsaidia," alisema Mtaturu.
Mtaturu akizungumzia shughuli za maendeleo
alisema baada ya miezi miwili ijayo kata hiyo itakuwa imepata umeme
kwani kazi kubwa anayoifanya mkandarasi hivi sasa ni kupeleka nyaya na kufunga
transifoma baada ya kufikisha nguzo.
Akizungumzia kuhusu miradi ya barabara alisema Rais Samia ametoa fedha kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya kilometa 460 ya kiwango cha lami ambapo ujenzi
wake unatarajiwa kuanza mara moja kuanzia Njiapanda, ambayo itapitia Makiungu,
Misughaa, kwa Mtoro hadi Kibrash mkoani Tanga.
Alisema hivi sasa unafanyika mchakato wa kumpata mkandarasi mwenye sifa ili
kazi hiyo ianze kufanyika na kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutainua uchumi
wa wananchi itakapita.
Kuhusu sekta ya kilimo alisema Wizara ya Kilimo chini ya Waziri Hussein
Bashe imeahidi kutoa mbegu za ruzuku za alizeti kwa ajili ya kuwasaidia
wakulima ili kuongeza uzalishaji na kuwainua kiuchumi.
Aidha, Mtaturu alisema Serikali imedhamilia kuliendeleza zao la kibiashara
la pamba kwa kuleta viatilifu na kuwa na bei nzuri na kuhakikisha barabara zote
zinazopita kwenye maeneo ya mashamba hayo zinapitika ili kusaidia kusafirisha
mazao hayo kwenda kwenye soko.
Mkuu wa shule hiyo Jackson Maruma alimshukuru mbunge huyo kwa msaada
alioutoa na kueleza kuwa sio mara yake kufanya hivyo kwani aliwahi kutoa
kompyuta tano lakini ni mbili tu ambazo zinatumika kutokana na kukosekana kwa umeme
na sasa tena ametoa projekta moja na kompyuta nne nyingine.
Pia mkuu wa shule hiyo alisema Mtaturu ameweza kufanikisha kupatikana kwa
mnara wa simu wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ambapo sasa wanapata huduma ya
intaneti katika kata nzima na shule hiyo ikinufaika kwa kufundishia wanafunzi
masomo mbalimbali.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Athuman Kitiku akizungumza wakati akitoa shukurani kwa mbunge huyo alisema maboresho yaliyofanywa katika shule hiyo hayawezi kumfanya mzazi ambaye mtoto wake anasoma hapo aweze kujuta na kuwa mbunge huyo anamchango mkubwa wa maboresho hayo.
0 Comments