Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Shafin Sumar Mwanamamlo (kushoto), akikabidhi, vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Milioni 28 kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma kwenye Zahanati za wilaya hiyo. Katikati ni Mbunge wa Jimbo la Igalula, Venant Protaus na kulia ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Winde Robert.
............................................
Na Moses Mabula Tabora
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa
Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Shafin Sumar
Mwanamamlo ametoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Milioni 28 kwa ajili ya
kusaidia kutoa huduma kwenye Zahanati za wilaya hiyo.
Vifaa hivyo amevikabidhi kwenye sherehe za
Umoja wa Wazazi ambayo imefanyika katika Kijiji Cha Mmale Kata ya
Miyenze wilayani humo Januari, 28, 2024.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa
Wazazi Mkoa wa Tabora, Robert Kamoga, Mwanamamlo alisema yeye kama kiongozi wa
jumuiya hiyo ameguswa na kwamba anatambua umuhimu wa afya ya kila mtu hivyo
akaona ni vema afanye hivyo ikiwa ni njia mojawapo ya kusaidia jamii hasa
katika upande wa afya.
"Mimi kama Mwenyekiti na kamati yangu ya jumuiya ya wazazi wilaya ya
Uyui, tumeona nivema tutoe vifaa hivi ili viweze kusaidia wajawazito wasipoteze
maisha yao kwa kukosa vifaa tiba," alisema Mwanamamlo.
Aidha, Mwanamamlo alisema kuwa CCM kupitia Mwenyekiti wake wa Taifa Dkt
Samia Suluhu Hassan kimefanya mambo
mengi makubwa ikiwemo ujenzi wa Zahanati vituo vya afya na madarasa ya shule za
Sekondari na msingi kwa nchi nzima.
Mwanamamlo aliwataka wananchi kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa
vile chama hicho kinatekeleza ahadi zake kama kinavyoahidi kwenye kampeni zake
wakati wa uchaguzi mkuu na kwamba ndio mkombozi kwao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Winde Robert alimshukuru Mwanamamlo na kamati yake kwa msaada huo na kuwa ni wajibu wa watumishi wa sekta ya afya kwenda kuvitunza ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu ukizingatia kuwa vifaa hivyo vinanunuliwa kwa fedha nyingi.
Vifaa tiba vilivyotolewa na Mwanamamlo ni viti mwendo vitatu vitanda kwa ajili ya kujifungulia wajawazito na taa zinazotumika wakati wajawazito wakijifungua.
0 Comments