Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Mika Likapakapa ,akihutubia wananchi na Wana CCM katika sherehe za kuadhimisha miaka 47 tang kianzishwe chama hicho Februari 5, 1977 zilizofanyika kiwilaya Kata ya Puma.
................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Mika
Likapakapa amesema wilaya hiyo inajivunia mafanikio lukuki yaliyopatikana
katika kipindi cha miaka 47 tangu kuzaliwa kwa chama hicho Februari 5, 1977.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 47 tangu kuzaliwa kwa
CCM yaliyofanyika kiwilaya Kata ya Puma Februari 3, 2024 alitaja baadhi ya
mafanikio wanayojivunia ni miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa na Serikali
kwa gharama kubwa si kwa Ikungi tu bali kwa nchi nzima ambapo alimtaka kila
kiongozi katika wilaya hiyo kuyatangaza mafanikio hayo ya Serikali ya kwanza
hadi ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili wananchi wayajue na
kuendelea kukiamini cha hicho.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya,
zahanati, maji, shule za sekondari na msingi, miundombinu ya barabara na kufikisha
umeme katika vijiji vyote isipokuwa vijiji sita tu ambavyo vitafikishiwa
Disemba mwaka huu.
Alisema ndani ya Kata 28 zilizopo kwenye wilaya hiyo kuna shule za msingi,
sekondari, vituo vya afya na zahanati zimejengwa na kuwa hapo awali wananchi
walikuwa wakilazimika kuchangia ujenzi wa shule hizo na ununuzi wa madawati.
Likapakapa alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wabunge Elibariki Kingu wa
Jimbo la Singida Magharibi na Miraji Mtaturu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa
kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea wana Ikungi maendeleo kwa kushirikiana na
madiwani wa wilaya hiyo pamoja na wataalamu mbalimbali.
Aidha, Likapakapa aliwahimiza wananchi kujishughulisha na kilimo, kusomesha
watoto, kutojiingiza katika mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji) na
kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwani mambo hayo ni kauli mbiu ya
CCM.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga alisema katika
kipindi hiki cha miaka 47 wanajivunia kuona Serikali ikitoa fedha nyingi za
miradi mbalimbali katika wilaya hiyo na kueleza kuwa katika awamu hii ya
Serikali ya awamu ya sita fedha nyingi zimemwagika kwenye miradi na kuwa
halmashauri hiyo siku zote imekuwa ikitekeleza maagizo ya Serikali na kuwa
imehimarika.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi Stamili Dendego akimkaribisha mgeni rasmi wa
sherehe hiyo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kufika
kwa wingi na kueleza kuwa sherehe hizo katika wilaya hiyo zimefanikiwa kutokana
na ushirikiano mkubwa baina ya viongozi na wananchi PAMOJA na wana CCM.
Dendego alisema katika maadhimisho hayo kazi mbalimbali zilifanyika
zikiwemo za kufanya usafi, kupanda miti kuzungunga Zahanati ya Kijiji cha Puma
na Shule ya Sekondari ya Puma, kugawa zawadi kwa wanafunzi wa shule hiyo ambapo
pia alipokelewa Joramu Ntandu aliyekuwa kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo
ambaye alihamia CCM.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akizungumza kwa niaba ya Mbunge mwenzake, Elibariki Kingu alisema katika kipindi hicho cha miaka 47 tangu tupate uhuru mwaka 1961 Tanzania imebadilika kwa kuwa na maendeleo makubwa hivyo tunakila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliletea Taifa maendeleo.Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Mika Likapakapa akishiriki kupanda mche wa miti katika eneo la la kituo cha afya cha Kata ya Puma ikiwa ni moja ya shughuli za sherehe hiyo.
0 Comments