………
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
IMEELEZWA kuwa zao la karafuu
ambalo kwa sasa linalimwa katika Mkoa wa Morogoro limetajwa kuwa miongoni wa
zao la kimkakati ambalo linatarajiwa kuongeza kipato cha mkulima sambamba na
ajira kwa wakazi.
Akizungumza
na waandishi wa habari mkoani hapa, Meneja wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo
Nyanda ya Juu Kusini (SAGCOT) Kongani ya Kilombero, John Banga amesema mbali
kuupaisha mkoa, kilimo cha karafuu ambacho kinalimwa pamoja parachichi ni mazao
yanayowavutia wakulima wengi.
“Wakulima wa karafuu mkoani hapa
wamekuwa wakilima kwa ustadi mkubwa sambamba na kupewa mafunzo na safari za
mafunzo Zanzibar ambako ni chimbuko la zao hili la karafuu katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,” amesema Banga.
Meneja huyo amesema kuwa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana SAGCOT imeshawapeleka wakulima
Zanzibar kujifunza namna bora ya kuendeleza kilimo cha Karafuu hapa nchini.
“Serikali imekuwa ikitoa msaada
wa taarifa za masoko, pembejeo, upatikanaji wa kifedha kwa wakulima na utoaji
wa mafunzo kupitia safari za visiwani Zanzibar ili kujifunza kwa wakulima
wenzao na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema.
Kwa mujibu wa Banga, Mkoa wa
Morogoro hususani katika wilaya zake za Gairo, Mvomero na Kilombero zimekuwa na
hali hewa nzuri pamoja na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha karafuu.
Amesema SAGCOT kupitia wabia wake
mbalimbali wakiwemo IUCN, AWF, WWF na wadau wengine wa maendeleo wamekuwa
wakishirikiana kwa karibu na wakulima katika kuboresha kilimo cha karafuu.
“Mwaka 2023, Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na SAGCOT waliwezesha ziara ya wakulima zaidi
ya 50 na wataalam wa mikoa ya Morogoro na Tanga kujifunza Zanzibar namna ya
kuongeza thamani kwenye mazao ya viungo ikiwemo karafuu,” amesema.
Amesema kufuatia ziara hiyo,
wadau walielekeza nguvu kwenye uzalishaji wa miche bora ya karafuu hadi mwezi
huu (Februari 2024), zaidi ya miche laki tatu na nusu imezalishwa katika Wilaya
ya Morogoro pekee ambapo miche hiyo inatarajiwa kupandwa kwenye mashamba ya
wakulima wadogo zaidi ya elfu tano.
Banga amesema Wilaya ya Gairo
pekee kuna zaidi ya wakulima 500 ambao wamehamasika kufanya kilimo cha karafuu
na wakulima zaidi ya 40 wameshapewa mafunzo maalumu ya kilimo cha kisasa cha
parachichi kutoka mkoani Njombe.
“ Tunategemea kupitia zao la karafuu mapinduzi makubwa ya kiuchumi na matokeo chanya katika kukuza pato la mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake ,” amesema Banga. nakuongeza kuwa zao hilo jipya linaratibiwa na SAGCOT kupitia Kongani yake Kilombero.
0 Comments