KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,Mary Maganga
amewataka wananchi wa Vijiji vya Magubike na Ilalasimba vilivyopo Kata ya Nzihi Halmashauri ya Iringa Vijijini, mkoani Iringa
kufanya
shughuli zisizoharibu mazingira ili kutunza
uoto wa asili wa maeneo hayo.
Maganga ameyasema hayo Februari 28, 2024 wakati
alipoongoza Ujumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na
Hifadhi ya Bioanuai (SLR) kukagua
shughuli za utekelezaji wa Mradi katika Kata ya Nzihi, Halmashauri ya Iringa
Vijijini, Mkoani Iringa.
Katibu Mkuu, Maganga ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mradi wa SLR, alikagua shughuli za hifadhi wa
mazingira katika Kata hiyo ikiwemo hifadhi ya msitu wa Kijiji cha Ilalasimba,
Shamba darasa la kilimo hifadhi, shamba darasa la malisho Kijiji cha
Ilalasimba, shughuli za ufugaji ng’ombe wa maziwa na hifadhi ya Kijiji cha
Magubike.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa uoto wa asili katika
maeneo yote ya Mradi, Serikali kupitia Mradi wa SLR imeunda timu ya Wataalamu
kutoka Wizara za Kisekta zikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Wizara ya Maji ikiwa ni mkakati mahsusi wa kurudisha
uoto wa asili uliopotea katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa sisi wa zamani sote ni mashahidi tunakumbuka hali
ya maeneo haya ilivyokuwa na uoto wake wa asili tofauti na hali ilivyo sasa…..Ili
kurejesha uoto wa asili wa eneo hili tumeleta Mradi huu wa SLR na matunda
yameanza kuonekana sasa, tunataka mradi huu uwe wa mfano tusimulie hadithi
nzuri kwa vizazi vyetu” alisema Maganga.
Aidha,Maganga ameipongeza Timu ya Watalaamu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuongeza kasi ya utoaji wa
elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi ikiwemo upandaji wa miti kwa mujibu
wa maelekezo ya Serikal ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maganga amesema kuwa ni muhimu
shughuli za kilimo, mifugo na misitu ziende sambamba na juhudi za kuhifadhi mazingira ili
kuhakikisha mradi huo unakuwa
endelevu na hivyo kuendelea kutunza uoto wa asili wa maeneo
hayo.
Aidha
ameridhishwa na mwamko wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya
mazingira, hatua iliyotokana na jamii hizo kuwa mstari wa mbele kusimamia
miradi katika kujikwamua kiuchumi na hivyo kuongeza pato la familia.
Amefafanua kuwa uoto wa asili sambamba na upandaji wa
miti pia unahusisha utumiaji wa rasilimali zilizopo kwa njia endelevu ikiwa ni
pamoja na kuacha maeneo yaliyoharibika kurejesha yenyewe uoto wake wa asili na
kuachana na shughuli zinazopelekea uharibifu ikiwemo ukataji miti.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SLR,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Bashir Muhoja alisema mradi
huo unatakelezwa katika Kata tatu ambazo ni Nzihi, Izazi na Migoli pamoja na
vijiji nane (8) ambapo kufikia Desemba 2023 Ofisi yake iliidhinishiwa kiasi cha
Sh. Milioni 426 kwa ajili ya utekelezaji.
Muhoja alisema kuwa shughuli zilizotekelezwa ni pamoja
na kukamilika kwa ujenzi wa josho na kibanio katika Kijiji cha Makuka,
kuwezesha vikundi vinne vya kijamii kutekeleza shughuli mbadala za ufugaji wa
ng’ombe wa maziwa, mbuzi na nyuki pamoja na kuwezesha upandaji miti na
kuanzisha mashamba darasa ya kilimo na mifugo.
“Hadi kufikia Desemba, 2023 kiasi cha Sh.Milioni 320.6
zilizopokelewa ambazo ni sawa na asilimia 75.19 na utekelezaji wa shughuli kwa
fedha za mwaka 2023 bado unaendelea. Shughuli zinazoendelea kutekelezwa ni
pamoja na kusambaza mtandao wa maji kwa wananchi wa Kata ya Migoli na miradi
mingine ya maendeleo,” alisema Muhoja.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR,
Dkt. Damas Mapunda kwa mujibu wa Dkt. Mapunda mradi huo ulianzishwa mahsusi
ikiwa ni juhudi za pamoja baina ya Serikali na wadau wa maendeleo ili kukabiliana
na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kunakosababishwa na shughuli za
kibinadamu ukataji miti, uchomaji mkaa na
uharibifu wa vyanzo vya maji.
Aliongeza kuwa mradi huo pia umekusudia kuandaa mpango
wa matumizi bora ya ardhi ili kuwezesha uboreshaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja
na malisho ya mifugo ili kuzuia
muingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo yaliyohifadhiwa
ikiwemo vyanzo vya maji.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephen
Mhapa ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ufadhili wa
miradi wa mazingira ambayo imebadili hali ya maisha ya kiuchumi kwa wananchi
wake na kuongeza kuwa halmashauri hiyo itahakikisha miradi hiyo inakuwa
endelevu.
“Tunachoahidi kwako katibu mkuu ni kuhakikisha mradi
huu unakuwa endelevu kwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo ili wawe mashuhuda wa jitihada
za hifadhi ya mazingira zilivyofanywa kwa ustadi mkubwa na jamii zilizopo katika
Vijiji vya Ilalasimba na Magubike” amesema Mhapa.
Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa
Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu
wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
huo.
Mradi wa SLR unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano
kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 kukamilika
mwaka 2025 ambapo jumla ya mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54
vinanufaika na mradi huo.
Halmashauri zinazonufaika na
mradi huo ni Halmashauri ya Iringa Vijijini (Iringa), Wilaya ya Mbeya na
Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na
Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga akisoma bango linaloonesha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa hifadhi ya msitu wa Kijiji cha Ilalasimba kilichopo Halmashauri ya Iringa Vijijini wakati wa ziara yake hiyo. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Stephen Mhapa.
0 Comments