Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Mwanashehe Jumaa wakati akikabidhi jenereta la dharura litakalotumika katika Kituo cha Afya Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida Februari 7, 2024
.................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekikumbuka Kituo cha Afya cha
Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kutoa fedha jumla ya
Sh.Milioni 150 kwa ajili ya kununua vifaa tiba.
Afisa Mauzo wa MSD Kanda ya Dodoma,
Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Mwanashehe Jumaa wakati wa kukabidhi jenereta
la dharura litakalotumika katika kituo hicho lenye thamani ya Sh.Milioni 65.7
alisema kati ya fedha hizo zilizotolewa tayari wamekwisha peleka vifaa vyenye
thamani ya Sh.Milioni 98.3.
"Vifaa vingine vilivyobaki vitaendelea kupelekwa hadi kufikia mwishoni
mwa mwezi huu MSD itahakikisha vinafika na vinatumika kutoa huduma za matibabu
kwa wananchi," alisema Mosi.
Alisema katika zoezi la kupeleka vifaa tiba hivyo kwenye vituo vya afya
Ofisi ya Rais TAMISEMI imetenga jumla ya Sh.Milioni 700 kwa ajili ya manunuzi
ya vifaa hivyo na kuwa Kituo cha Afya Msange kimenufaika na fedha hizo.
Alisema katika Halmashauri hiyo vituo sita vimetengewa fedha kwa ajili ya
vifaa hivyo ambavyo vinaendelea kupokelewa.
Mosi alisema jukumu kubwa la MSD ni kununua, kutunza, kuzalisha dawa, vifaa
tiba na vitendanishi vya maabara katika vituo vyote vya Serikali vilivyopo
nchini na kueleza kuwa MSD wamedhamiria kuokoa maisha ya watu.
Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Singida, Eliya Digha akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo alimshukuru
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watanzania hususani wananchi wa
halmashauri hiyo na Kata ya Msange.
Alisema kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Serikali jumla ya Sh.Milioni
500 na kuwa wametumia Sh.Milioni 200 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa tiba.
Digha aliishukuru Serikali na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo la dharura
ambalo linakwenda kusaidia wakati umeme utakapokuwa unakatika.
Wakazi wa Kata hiyo Hamisi Ramadhani na Greta Nyonyi waliishukuru Serikali
na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo ambalo litakuwa mkombozi kwao.
"Tulikuwa na changamoto kubwa baada ya umeme wa kawaida kukatika hasa
kwa upande wa wajawazito ambao walikuwa wakitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini
kwa jenereta ili tuliloletewa na MSD tuna kila sababu ya kutoa shukurani zetu
kwa viongozi wetu," alisema Nyonyi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau alisema jenereta hilo litawafanya kuwa na umeme wa uhakika na kuweza kutoa huduma za matibabu kwa urahisi na haraka kwa masaa 24.Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau akizungumza wakati wa mapokezi hayo.
0 Comments