MAZISHI YA MKE WA MCHUNGAJI YAACHA HISTORIA SINGIDA

Subscribe Us

MAZISHI YA MKE WA MCHUNGAJI YAACHA HISTORIA SINGIDA

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Bibi Elizabeth  Mwamkumbi Kimoho (96) .
.....................

Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog

VILIO Simanzi na huzuni vilitawala katika ibada ya mazishi ya Bibi Elizabeth  Mwamkumbi Kimoho (96) Mkazi wa Kijiji cha Ihanja Wilayani Ikungi mkoani Singida ambaye imeelezwa kuwa yeye pamoja na mume wake Marehemu Andrew Duma aliyekuwa  Mchungaji wa Kanisa la The Free Pentecostal Church of Tanzania Jimbo la Singida ni waasisi wa kanisa hilo katika kijiji hicho na wakuu wa imani ya Mungu.

Askofu wa kanisa hilo  Jimbo la Ikungi, Mchungaji Yeremia Samwel akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika Februari 12, 2024 katika Kanisa la FPCT Parishi ya Ihanja alisema Elizabeth na mume wake Andrew Duma walikuwa ni wakuu wa Mungu kutokana na kazi kubwa walioifanya ya kueneza imani katika kijiji hicho na Singida kwa ujumla.Askofu wa Kanisa la FPCT,  Jimbo la Ikungi, Yeremia Samwel .

---------------

"Bibi huyu ambaye tunamuaga leo hapa alikuwa akisaga mahindi na mboga kavu za majani kwa kutumia jiwe la asili na kuandaa chakula kwa ajili ya wachungaji walipokuwa kwenye vikao na mikutano mbalimbali," alisema Mchungaji Samwel..

Samwel alisema Bibi Elizabeth ni  mke wa kwanza wa mchungaji ndani ya kanisa hilo katika Mkoa wa Singida na kupitia utumishi wao pamoja na mume wake wameweza kuzalisha maaskofu na wachungaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida hasa katika majimbo yao matatu ya Ikungi, Irongelo na Singida mjini.

Alisema mbali ya kuzalisha watumishi wengi ndani ya Mkoa wa Singida pia walifanikisha mchungaji waliokuwa wakimlea kiimani  kwenda kuanzisha huduma mkoani Iringa ambapo kwa sasa ni Askofu wa kwanza wa kanisa hilo mkoani humo.

"Ninamfahamu vizuri bibi huyu alikuwa hana maneno mengi na alikuwa mkarimu kwa wageni na alipokuwa akipita maeneo ya Ikungi ambayo wakati huo hayakuwa na kanisa hata moja alikuwa akisikitika huku apaza sauti ya kuomba kuanzishwa kwa kanisa haraka ili watu wamjue Mungu, alisema Samwel.

Samwel alisema kuwa Bibi Elizabeth hajafa bali amelala kama alivyolala Mfalme Daud anayetajwa kwenye biblia na kuwa ipo siku ataamka.

Aidha, Samwel aliwataka wakristo kumuenzi bibi huyo kwa kufanya mambo mazuri ya kumpendeza Mungu hasa akawaomba wanafamilia yake hasa wajukuu kufuata nyayo zake.Makamu Askofu wa kanisa hilo, Jimbo la Ikungi, Mchungaji Simoni Jingu, akizungumza kwenye ibada hiyo.Askofu Amosi Maghasi

/////////

Askofu Amosi Maghasi wa kanisa hilo Jimbo la Singida aliwataka wakristo kuendelea kujiandaa  na kuwa watu wema na watakatifu kama alivyokuwa bibi Elizabeth na alitumia nafasi hiyo kuwaomba waandishi wa habari si kuandika habari nzuri tu za wanasiasa kwa ajili ya kulipwa mishahara bali pia waandike habari njema za Mungu.Waandishi wa habari Mkoa wa Singida wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Bibi Elizabeth Kimoho.Askofu wa Jimbo la Ilongero, Abdoni Samsoni.

------------------

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Irongero, Abdoni Samsoni alisema watu wote waliokuwepo kwenye ibada hiyo na wengine wote wana jambo la kujifunza kupitia kifo cha Bibi Elizabeth kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya.

Askofu Mstaafu , Wilson Lazaro
---------

Askofu Mstaafu wa kanisa hilo Jimbo la Irongelo, Wilson Lazaro alisema wakristo wana kila sababu ya kuendelea kujifunga mkanda kwa kuyaenzi mambo yote mazuri aliyokuwa akiyafanya bibi Elizabet Kimoho ambaye mwisho wa maisha yake hapa duniani ameumaliza vizuri.

 Lazaro alitumia nafasi hiyo kuiomba jamii na wakristo kuendelea kuwa na imani na kufanya mema kama alivyokuwa akifanya Mchungaji Duma na mke wake jambo litakalosaidia nchi kuwa na utulivu na amani.

Aidha, Askofu Lazaro alitumia nafasi hiyo kutoa nasaha kwa jamii kuwajibika kuwatunza wazee kwani hata wao ni wazee watarajiwa wa kesho na kuwa kifo kipo kwa kila mmoja changamoto iliyopo ni kujua ni nani atatangulia hilo ndio fumbo kubwa la Mungu.

Askofu Mstaafu, Jacob Nyika
---------

Askofu Mstaafu, Jacob Nyika alisema marehemu Mchungaji Andrew Duma na mke wake Elizabeth Kimoho wamefanya kazi kubwa ya kueneza imani hivyo wanawajibu wa kuwaenzi kwa kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano katika majimbo yao yote hayo matatu kuanzia ngazi ya maaskofu hadi wachungaji.Diwani wa Kata ya Ihanja, Mohamed Igae 

-----------

Kwa upande wa viongozi wa Serikali Diwani wa Kata ya Ihanja, Mohamed Igae  na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Juma Memba wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ibada hiyo wakati wakitoa salamu za rambirambi kwa wafiwa waliiomba jamii kuyaenzi yale yote mazuri yaliofanywa na watumishi hao wa Mungu Elizabeth na marehemu mume wake Mchungaji Andrew Duma.Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihanja, Juma Memba

----------

Viongozi hao kupitia Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Ihanja walitumia fursa ya ibada hiyo kuwaomba wananchi kuwapeleka watoto wao waliochini ya umri wa miaka mitano kupata chanzo ya Surua itakayoanza Februari 15, 2024 hadi Februari 18, 2024.

Akisoma historia ya marehemu Mchungaji Elikana Mkuki wa Kanisa hilo Kijiji cha Ihanja, alisema Bibi Elizabeth Mwamkumbi Kimoho alizaliwa Mei 2, 1928 katika Kitongoji cha Misake Kijiji cha Minyughe Wilaya ya Ikungi Singida.Mchungaji, Elikana Mkuki 

-----

Alisema Marehemu alifunga ndoa ya kimila mwaka 1944 na Andrew Duma ambapo walijaaliwa kupata watoto tisa, waliofariki ni watatu wakiume wawili na wa kike mmoja na ambao wapo hai ni  sita wakike watatu na wakiume watatu,  mmoja wao ni Mwandishi wa habari Mkoa wa Singida, Nathaniel Limu.

Akizungumzia suala la imani alisema marehemu aliokoka mwaka 1964 katika Kanisa la FPCT Parishi ya Ihanja na alianza utumishi wake na mume wake Andrew Duma mwaka 1965 na waliteuliwa kuwa wachungaji mwaka 1969.

Mchungaji Mkuki alisema walifanya kazi ya utumishi Kijiji cha Minyughe, Mtamaa, Singida mjini, Sagara na maeneo mengine mbalimbali ndani ya Mkoa wa Singida.

Waombelezaji wakiwa kwenye ibada hiyo
----------

Mchungaji Mkuki akizungumzia maradhi ya marehemu kuwa alianza kuugua mwaka 2022 baada ya kuvunjika mguu na tangu hapo hali yake ya kiafya iliendelea kutetereka ambapo alipelekwa Hospitali mbalimbali kwa ajili ya matibabu lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya kutokana na maumivu ya mguu na Februari 9, 2024 majira ya saa 3 na nusu asubuhi alifariki dunia.

Marehemu ambaye alikuwa na umri wa miaka 96 ameacha watoto sita, wajukuu 13 na vitukuu 14. 

Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake libarikiwe.


Waombolezaji wakienda kutoa heshima ya mwisho kwa mwili wa marehemu.
Kwaya ya Mwangaza ikiimba nyimbo za maombolezo.
Wachungaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
Familia ya marehemu ikijumuika kwenye ibada ya kumuaga mpendwa wao.
Kwaya ya Sinai ikiimba nyimbo za maombolezo kwenye ibada hiyo.
Huzuni ukitamalaki kwenye ibada hiyo.
Wake za wachungaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
Taswira ya ibada hiyo.
Viongozi wa Taasisi ya Catherine Foundation ambayo ilikuwa ikimsaidia marehemu Elizabeth Kimoho kwa mahitaji mbalimbali na huduma ya kiroho wakitoa salamu za rambirambi. Kutoka kushoto ni Kiongozi wa Taasisi hiyo Rehema Sungu, Mweka Hazina wa Taasisi hiyo, Joyce Gunda na Mchungaji Peter Paul Samwel Mlezi wa Taasi hiyo.
Waombolezaji wakitoa heshima kwenye jeneza lenye mwili wa marehemu.
Ni vilio baada ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Askofu wa Kanisa la FPCT Singida Mjini, Dkt.Paul Samwel ambaye aliwahi kuwa Makamu Askofu Mkuu   wa Kanisa la FPCT akizungumza kwenye ibada hiyo.
Katibu wa kanisa hilo Jimbo la Ikungi, Philip Sospeter akiongoza itifaki wakati wa ibada hiyo.
Ibada ya kuaga mwili wa Elizabeth Kimoho ikiendelea.Muonekano wa Kanisa la Free Pentecostal Tanzania la Kijiji cha Ihanja lililoasisiwa na  marehemu Elizabeth Kimoho na Mume wake Andrew Duma ambao wamepewa heshima ya kuzikwa kwenye makaburi ya kanisa hilo.
Marehemu Bibi Elizabeth  Mwamkumbi Kimoho (96) enzi za uhai wake.


Post a Comment

0 Comments