.........................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
JUMLA ya watu 1404 wameathirika na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha
katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambapo nyumba 351 zikiwa zimezingirwa
na maji na vyoo 368 kubomoka.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu athari zilizosababishwa na mafuriko hayo alisema kaya 368 zimeathiriwa
na mafuriko hayo na kuwa nyumba 17 zimebomoka na kueleza kuwa Serikali
imeendelea kuchukua hatua za kuwasaidia waathirika.
Shaka alitaja maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo kuwa ni Kitongoji cha
Kampala kaya 161 na watu 624 wameathirika, Kitongoji cha Madizi kaya 137
zimeathirika na watu 531, Kitongoji cha Estate kaya 57 na watu 196
wameathirika.
Alitaja vitongoji vingine kuwa ni cha Lugunga Kata Nane na watu 32
wameathirika na Kitongoji cha PWD kaya tano na watu 20 wameathirika.
Shaka alisema kati ya nyumba 17 zilizobomoko tano zipo Kitongoji cha
Kampala, nyumba nane Kitongoji cha Estate na nyumba nne Kitongoji cha Madizini.
Alisema jumla ya vyoo 368 vimeathirika na
kusababisha maji kuwa machafu baada ya kusombwa na maji ya mafuriko hayo
na kuvibomoa ambapo jumla ya visima 30 vya maji vimeathirika kwa kuingiliwa na
maji machafu.
Akizungumzia kuhusu miundombinu ya barabara alisema zaidi kilometa 170 za
barabara zimeathiriwa na maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya
Kilosa na Mikumi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi ambao wanatumia
barabara hiyo kwa shughuli za usafiri.
Alisema Machi 17 mwaka huu maji mengi yalijaa katika mto Miyombo unaopita katika vijiji vya Ulaya,
Zombo na Changarawe baada ya mvua kubwa kunyesha katika vijiji vya Kisanga,
Madizini na Kitunduweta.
Alisema mvua hiyo ilisababisha athari katika makazi, mashamba na
miundombinu ya maji na barabara katika maeneo hayo na kuwa Kijiji cha
Changarawe kimekuwa na matukio ya kupatwa na mafuriko mara kwa mara tangu mwaka
2016 na msimu huu wa mvua kuanzia mwezi wa
Desemba mwaka jana hadi sasa ni tukio la tisa la mafuriko.
“Mafuriko haya yamesababishwa na maji kujaa katika Mto Miyombo baada ya
ongezeko la kujaa mchanga katika mabwawa
ya Nara na Kipera ambayo yalichimbwa kwa ajili ya kupunguza kasi ya maji
kipindi cha mvua kubwa na kuruhusu maji machache kuingia katika mto
huo,”alisema Shaka.
Shaka alisema uharibifu wa tuta
katika mto huo lililojengwa kuzuia maji yasiingie kwenye mashamba ya mkonge
enzi hizo ambayo sasa yamekuwa ni makazi ya watu na shughuli za kibinadamu kama
kilimo,mifugo ndio yanayosababisha madhara
hayo.
Shaka alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
namna anavyoguswa na hali ya mafuriko katika Wilaya hiyo ambapo nyakati zote
amekuwa akielekeza hatua mbali mbali za
haraka na dharura ili kuokoa maisha ya wananchi lakini pia kurudisha huduma za
kibinadamu.
"Tokea Disemba hadi leo tumekuwa na mafuriko ya mara kwa mara na Rais wetu amekuwa nasi nyakati zote tumepokea msaada wa chakula cha dharura, matibabu, magodoro lakini pia fedha za mfuko wa dharura katika kurudisha miundombinu ya barabara wananchi wanamshukuru sana vinginevyo hali ingekuwa tete kwani majanga haya yanakuja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hakuna anaeyatarajia ila Serikali imekuwa makini kuhakikisha tunakabiliana nayo," alisema Shaka.
0 Comments