.................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
MKUU wa Wilaya ya Tanga, James Wilbert Kaji amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ambao utaanza mbio zake leo Aprili 14, 2024 utatembea na kukagua miradi yenye thamani ya Sh.Bilioni 11 ambayo imetekelezwa mkoani humo.
DC. Kaji aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana kuhusu mbio hizo za Mwenge pamoja na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo amehimiza wananchi wenye sifa za kugombea uongozi kujitokeza kugombea.
Aidha Kaji aliwataka waandishi wa habari, kutumia kalamu zao kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo wa serikali za mitaa 2024 ambao ni wa muhimu kwa kuwapata viongozi.
Mkuu huyo wa wilaya akizungumzia mapokezi
ya Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, alisema utapokelewa leo April
14, 2024 ukitokea wilayani Mkinga.
"Tutaupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkinga,
utapitia miradi kadhaa ila niwaombe pia mtumie nafasi zenu kuhamasisha wananchi
kuuusu uchaguzi serikali za mitaa, mafanikio ya nchi na wananchi ni kuchagua
Viongozi wanaofaa, watakaosaidia kutatua kero" alisema DC Kaji.
Kwa mujibu wa Kaji, katika Wilaya ya Tanga Mwenge
wa Uhuru utapitia miradi nane (8) yenye thamani ya Shilingi 11,498,787,209
bilioni.
Pia Mwenge huo utahamasisha shughuli mbalimbali
kama vile mapambano ya VVU na UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na mapambano
dhidi ya viyendo vya rushwa.
Shughuli nyingine zitakazofanywa na Mwenge wa
Uhuru ni uhamasishaji lishe bora, kukagua namna Jiji linavyotunza mazingira na
kudhibiti taka na taka ngumu kwenye dampo la kisasa lililopo eneo la Mpirani na
kupanda miti ya matunda 50.
Utafungua mradi wa maji uliogharimu Shilingi
235,201,500 huko mtaa wa Putini, kutembelea vijana waliokopeshwa Mil 20 na
Halmashauri ya Jiji la Tanga ili kuendesha kituo cha kuosha na ukarabati mdogo
wa magari Mkwakwani youth centre.
Vilevile utazindua mradi ufuaji umeme wa jua
kiwanda cha PPTL wenye thamani ya Shilingi 6,760,000,000, kufungua madarasa
manne shule ya msingi Majengo mradi uliogharimu Tshs 100,000,000.
Mkuu huyo wa wilaya alioendelea kutaja shughuli
nyingine kuwa ni ukaguzi madarasa mawili na ofisi Mnyanjani shule ya msingi
mradi wenye thamani ya Shilingi 50,000,000.
Pamoja na hayo, klabu ya wapinga rushwa na dawa
za kulevya itafunguliwa huku taarifa mbalimbali ikiwemo ile Halmashauri ya jiji
la Tanga jinsi inavyojiandaa na uchaguzi Serikali za mitaa 2024 zitapokelewa.
Mengine ni mradi wa Zahanati ya Mzingani
unaogharimu Shilingi 150,000,000 kuwekwa jiwe la msingi, kupokea taarifa
mapambano dhidi ya malaria na ukaguzi barabara ya askari na lumumba yenye
thamani ya Shilingi 1,249,471,144 ikiwa ni ukaguzi endelevu wa miradi
iliyowekewa mawe ya msingi kwa mwaka 2023.
Aidha Mwenge wa Uhuru utafungua barabara ya Jumbe
na Dunia Hoteli yenye urefu wa kilomita 1.2 huku ukigharimu Shilingi
817,114,656.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 inasema "Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu ". Mkesha wa Mwenge utafanyika viwanja vya sekondari ya Usagara Jijini Tanga.
0 Comments