MBUNGE IRAMBA MASHARIKI ASHIRIKI BARAZA LA IDD KWA KUCHANGIA UJENZI WA ZAHANATI

Subscribe Us

MBUNGE IRAMBA MASHARIKI ASHIRIKI BARAZA LA IDD KWA KUCHANGIA UJENZI WA ZAHANATI

Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Francis Isack Mtinga (katikati) akishiriki Baraza la Eid El-Fitri lililofanyika Kata ya Tumuli wilayani Mkalama Aprili 12, 2024. Kushoto kwake ni Sheikh wa Wilaya ya Mkalama, Alhajj Miraji Ibrahim na kulia kwake ni Diwani wa Kata ya Tumuli, Bilal Msengi.

...........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)

MBUNGE wa Jimbo la Iramba Mashariki Francis Isack Mtinga ameshiriki Baraza la Eid El-Fitri na kuchangia ujenzi wa Zahanati  kwa kutoa baadhi ya vifaa vya ujenzi  na kupongezwa na wananchi pamoja na waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria baraza hilo.

Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Alhajj Miraji Ibrahim akizungumza wakati akimkaribisha Mbunge Isack Mtinga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa baraza hilo lililofanyika Aprili 12, 2024 Kata ya Tumuli alimshukuru mbunge huyo kwa kuacha shughuli zake na kwenda kujumuika nao katika jambo hilo kubwa la kiimani.

Sheikh Ibrahim alisema anatambua kuwa shughuli za mbunge ni pamoja na kuhudhuria vikao vya bunge kwa ajili ya kuwatafutia wana Mkalama maendeleo mbalimbali sanjari na mambo mengine.

"Tunakushukuru mbunge wetu kwa kazi kubwa uliyoifanya na unayoendelea kuifanya katika jimbo letu kwa kutuletea maendeleo hakika wewe ni jembe na Mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya na maisha marefu," alisema Ibrahim.

Alisema katika kipindi cha uongozi wake wa zaidi ya miaka mitatu Mbunge Mtinga ameweza kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya afya, kilimo na mingine mingi jambo ambalo wana Mkalama wanajivunia.

Mbunge Mtinga akizungumza katika baraza hilo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimetumika kutekeleza miradi hiyo na kuwa wana Mkalama hawana cha kumlipa zaidi ya kumpa kura nyingi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

"Sisi wana Mkalama hatuna cha kumpa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na maendeleo aliyotuletea katika jimbo letu zaidi ya kumpa kura nyingi za kutosha," alisema mbunge Mtinga.

Baada ya kufanyika kwa baraza hilo la Eid El-Fitri Sheikh wa wilaya hiyo Miraji Ibrahim pamoja na Mbunge Mtinga na viongozi mbalimbali na baadhi ya waumini wa dini ya kiislam na wananchi walikwenda kuomba dua katika jengo la Zahanati Mpya ya  Kata ya Tumuli inayojengwa kwa nguvu na michango ya wananchi wa kijiji hicho ambapo mbunge huyo alitoa mchango wa mifuko 200 ya  saruji na mbao za kupaulia jengo lote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 9.

Sheikh Ibrahim alisema bado wanahitaji michango zaidi ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo hivyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia ili kukamilisha ujenzi huo haraka iwezekanavyo wananchi waweze kuanza kupata huduma

Aidha,Sheikh Ibrahim alimuomba mbunge huyo kusaidia kununua gari ambalo litatumika kwa ajili ya matumizi ya shughuli za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wilayani humo na kuwa wao tayari wana kiasi cha Sh.Milioni 2.

Mbunge Mtinga alikubali ombi lao na kuomba kuundwa kwa kamati ya manunuzi ya gari hilo ambapo yeye atakuwa ni mwenyekiti.

Mtinga alisema katika wilaya hiyo kuna misikiti ya Ijumaa 110 ambayo ipo chini ya BAKWATA  ambapo aliomba kila msikiti kutoa Sh.100,000 hadi ifikapo Julai 30, 2024 na Sheikh atakayeshindwa kupata kiasi hicho cha fedha ndani ya muda huo  aondolewa kwenye uongozi na kupewa nafasi hiyo mtu mwingine.

Alisema baada ya kukusanya fedha hizo jumla ya Sh.Milioni 11 zitapatikana na kiasi kingine cha fedha kitapatikana kwa kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo na kuwa lengo lao ni kununua gari la kisasa badala ya Noa waliokuwa wakilihitaji ambayo kwa sasa imepitwa na wakati.

Mtinga alisema anaamini kama mchakato huo utaenda vizuri gari hilo watalikabidhi Bakwata Wilaya ya Mkalama wakati wa Sikukuu ya Maulid ya Kuzaliwa kwa  Mtume Muhammad (S.A.W) ambapo waislamu nchini  wataungana na wenzao duniani kuadhimisha siku hiyo muhimu katika Imani ya dini ya Kiislamu. itakayofanyika mwezi  Desemba, 2024.

Mazungumzo yakifanyika kabla ya kufanya dua kwenye jengo la zahanati hiyo.

Ukaguzi wa ujenzi wa zahanati hiyo ukifanyika.
Waumini wa dini ya Kiislam wakiwa kwenye baraza hilo la Idd.
Taswira ya baraza hilo. (Picha zote kwa Hisani ya Mohamedi Imbele)
 

Post a Comment

0 Comments