................................
Na Munir Shemweta, Mlele
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemuomba Mkuu wa wilaya ya
Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga kuunda Tume ya Kupitia Mapato na Matumizi ya fedha za
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika halmashauri ya Mpimbwe ili
kubaini kama kuna ubadhilifu basi wahusika wachukuliwe hatua kali.
Aidha, amemuomba mkuu huyo wa wilaya ya Mlele
kuchunguza kiasi cha fedha milioni 44 kilichotolewa na Mkandarasi anayejenga
barabara ya Kibaoni hadi Sitalike zinazodaiwa kulipwa kwa kijiji bila kufuata
utaratibu.
Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti
tarehe 12 April 2024 wakati wa mikutano yake ya hadhara na wananchi wa vijiji
vya Mirumba, Ilalangulu na Kibaoni katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya
Mlele mkoa wa Katavi.
Kauli Mhe. Pinda inakuja mara baada ya
kubadilishwa uongozi wa Kamati ya Kusimamia WMA ndani ya mwezi mmoja tu kamati
ilifanikiwa kukusanya shilingi milioni 200 tofauti na kamati iliyokaa kwa zaidi
ya miaka kumi na kudaiwa kutosaidia maendeleo yoyote ya vijiji husika.
"Iundwe tume ya kupita kitabu kwa kitabu
tujue miaka 20 fedha zetu zilienda wapi za wananchi hao, wiki mbili milioni 200
hebu tuwaulize miaka 20 wameleta nini?" Alihoji Mhe. Pinda.
"Pia kuna ubadhilifu wa milioni 44
zilizotolewa na mkandarasi anayejenga barabara ya kiabaoni- Sitalike ambaye
amelipa fedha kwa kijiji bila utaratibu. Uchunguzi nani amechukua fedha taslimu
ambazo hazijulikani zilipokwenda wapi ufanyike". Amesema Mhe. Pinda.
Aidha, ameuelezea mpango wa WMA kama wenye faida
kubwa kwa vijjji vinavozunguka hifadhi na kutolea mfano wa wilaya ya Tanganyika
kama wilaya inayonufaika na mpango huo ambapo kwa mujibu wa Mhe. Pinda mwaka
huu wa 2024 vijiji vinavyozunguka hifadhi vinaenda kupokea shilingi bilioni 16
.
Amesema kuwa, kiasi chochote cha fedha
kitakachopatikana kupitia mpango wa WMA lazima wananchi wahusishwe matumizi
yake ili fedha zinazokusanywa ziende kutumika kwenye shughuli za maendeleo ya
vijiji husika.
Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji
Majid Mwanga ameahidi kuunda haraka Tume itakayohusisha vyombo vya ulinzi na
usalama kama vile TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Magereza ili kubaini kama upo
ubadhilifu wowote wa fedha za umma basi wahusika waweze kuchukuliwa hatua
stahiki.
"Hakuna atakayepona katika suala hilo na
lazima tutawashughulikia wahusika wote waliowaibia wananchi. Kazi hii tunaiweza
na hatutacheka na mtu hata mmoja".
Amesema Alhaji Mwanga.
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele inahusisha vijiji vya Kibaoni, Mirumba, IIalangula pamoja na kijiji kimoja kutoka wilaya ya Nkasi. Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga akizungumza wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda katika kijiji cha Mirumba halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.
0 Comments