Mahakama kuu ya Huye kusini mwa Rwanda imemhukumu Beatrice Munyenyezi (pichani) kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya Kimbari.
Hakimu alisema kuwa Munyenyezi mwenyewe ana
jukumu kubwa katika mauaji ya kimbari na ubakaji wa wanawake na wasichana
katika mji wa Butare wakati wa mauaji ya kimbari.
Beatrice Munyenyezi alirudishwa nchini Rwanda na
nchi ya Marekani mwaka wa 2021 ili kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya kimbari.
Mawakili wake walitangaza kwamba watakata rufaa
kupinga uamuzi huo.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo leo Ijumaa
wahusika wote walikuwa mahakamani, mahakama ilimtia hatiani Munyenyezi kwa
makosa 4 yakiwemo mauaji ya kimbari na kuchochea ubakaji wa wanawake na
wasichana.
Hakimu alisema kuwa Beatrice Munyenyezi alihusika
moja kwa moja katika mauaji ya baadhi ya Watutsi katika mji wa Butare ambao
sasa ni mji wa Huye , akiwemo mtawa mmoja aliyeuawa na Munyenyezi mwenyewe kwa
kutumia bastola baada ya kubakwa na askari kwa amri ya mshtakiwa.
Hakimu alisema kuwa maelezo ya mashahidi katika
mauaji ya mtawa huyo hayana shaka.
Kadhalika Munyenyezi alishtakiwa kwa kufanya
mauaji akishirikiana na mumewe Sharom Ntahobari na mama mkwe wake Pauline
Nyiramasuhuko ,ambaye alikuwa Waziri wa Familia, wote wawili walifungwa Arusha
nchini Tanzania baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mauaji ya kimbari.
Katika utetezi wake wa mashitaka yanayomkabili
katika kesi hiyo, Beatrice Munyenyezi alisema waliotoa ushahidi dhidi yake
walisema uongo na ushahidi wao ulikuwa na utata.
Munyenyezi,54, alisema wakati wa mauaji ya
kimbari alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha na alikuwa na mtoto mdogo na
hivyo hangeweza kujihusisha na mauaji kwa kuwa hakuwa na nguvu.
Hoja yake hiyo ilipingwa na hakimu aliyesema
kwamba kuwa mjamzito hakuwezi kumzuia kutoa amri ya kuuwa na kwamba mahakama
haikupata ripoti ya daktari inayothibitisha kwamba alikuwa mgonjwa au dhaifu.
Awali katika kesi hii,Munyenyezi alisema kuwa
kesi yake ilichochewa kisiasa kwa sababu aliolewa katika familia iliyotiwa
hatiani kwa makosa ya mauaji ya kimbari akisisitiza kwamba ‘’siyo haki
kuadhibiwa kwa makosa ya wanafamilia wake’’
Mahakama ilimtia hatiani kwa makosa 4 kati ya 5
aliyoshtakiwa.
Pamoja na hayo, Hakimu alisema kuwa mmoja wa
majaji 3 alikuwa na maoni “tofauti ‘’ juu ya uamuzi huo, lakini hakuwa na mengi
ya kusema kuhusu hilo.
Munyenyezi alisema kuwa “hakushangazwa na uamuzi huo”, huku mawakili wake wakitangaza kwamba watakata rufaa haraka iwezekanavyo.
0 Comments