WATU TISA WAFARIKI KWA AJALI YA BASI SIKUKUU YA IDD SINGIDA

Subscribe Us

WATU TISA WAFARIKI KWA AJALI YA BASI SIKUKUU YA IDD SINGIDA

Wananchi wakiangalia ajali ya basi lililogonga lori lenye namba za usajili T485DBR /231DSE mali ya kampuni ya Glenrich  Transportation LTD liyotokea Aprili 10,2024 majira ya saa 11:00 asubuhi katika Kijiji cha Malendi Kata ya Mgongo Tarafa ya Shelui Wilaya ya Iramba Mkoa wa singida. 

 .........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog) 

WATU 9 wamefariki dunia  baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kuligonga lori la mizigo lililokuwa zimeegeshwa barabara kwa matengenezo baada ya kuharibika. 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pipi Kayumba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa waliofariki ni watu hao 7 wakiwemo wanaume 6 na mwanamke mmoja na wengine 8  kujeruhiwa  katika ajali hiyo iliyotokea Aprili 10,2024 majira ya saa 11:00 asubuhi katika Kijiji cha Malendi Kata ya Mgongo Tarafa ya Shelui Wilaya ya Iramba Mkoa wa singida. 

Kayumba alisema ajali hiyo imehusisha Basi aina ya  Yutong lenye namba za usali T.315CXX  linalomilikiwa na Kampuni ya Lujiga Express lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye ametoroka baada  ya ajali hiyo kutokea na kusababisha vifo hivyo. 

" Basi hilo liligonga lori aina ya DAF lenye namba za usajili T485DBR /231DSE mali ya kampuni ya Glenrich  Transportation LTD likiendeshwa na dereva aitwaye Mohamed Ally (52) mkazi wa Sinza –Dar es salamu ambaye aliliegesha lori hilo pembezoni mwa barabara kwa ajili ya matengenezo," alisema Kamanda Kayumba. 

Aidha, Kamanda Kayumba alisema uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali ni mvua iliyokuwa inanyesha ikiambatana na ukungu na dereva wa basi kutokuwa makini na kushindwa kuchuki\ua tahadhari wakati analipita gaari liliokuwa limeharbika.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya uchunguzi na majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na Hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa ajili ya kupatiwa matibabu..

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Daniel Paul alisema walipokea miili saba ya watu waliofariki katika ajali hiyo na majeruhi wakiwa 19 ambao walikuwa wakipatiwa matibabu Hospitali za Wilaya ya Igunga na katika Hospitali ya Wilaya ya  Iramba wakiwa watatu akiwepo mjamzito ambaye walilazimika kumfanyia upasuaji na kukuta mtoto wake akiwa amefia tumboni.

Alisema mama huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo na hali yake inaendelea vizuri lakini majeruhi wawili waliokuwa pamoja na mama huyo kutokana na hali zao kuwa mbaya walifariki wakati wakipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Singida na kufanya idadi ya waliofariki katika ajali hiyo kuwa tisa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linatoa wito kwa wananchi kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora ili kutambua marehemu na linatoa wito kwa madereva kuzitii na kuziheshimu sheria za barabarani  kuepuka ajali zinazoweza kusabibisha majeruhi, vifo au uharibifu kwa vyombo husika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida katika kubaini, kutanzua na kuzuia uhalifu limeendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wanachi kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yote ya mkoa.

Askari wa usalama barabarani wakiangalia ajali hiyo.
Muonekano wa basi hilo baada ya kuligonga lori hilo.
Askari wa jeshi la polisi wakijadiliana jambo katika eneo la ajali.
Malori yakiwa katika foleni baada ya magari yaliyopata ajali kuzuia barabara.
Muonekano wa basi hilo kwa nyuma baada ya ajali.
Katikati (kushoto) ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pipi Kayumba na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara Mkoa wa Singida, Mrakibu wa Polisi (SP) Nestory Didi wakipata maelezo kutoka kwa abiria waliokuwa wamepanda basi hilo ambao walisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo mbaya na dereva kuwa na usingizi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Vicktorina Ludovick akizungumza na abiria waliokuwa wamepanda basi hilo. 

Post a Comment

0 Comments