TAASISI ZA KIISLAMU MKOA WA SINGIDA ZITAKAZO BAINIKA KUIBA WANYAMA WA SADAKA KUFUTIWA KIBALI
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro akizungumza na Waislamu wanaojishughulisha na wasimamizi wa Taasisi zinazojishughulisha na uchinjaji wa wanyama wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Eid ul Adha uliofanyika Mei 3, Ofisi ya Baraza Kuu la Waislamu Mkoa wa Singida.
.......................................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
SHEIKH wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro ametoa
onyo kwa Taasisi za Dini ya Kiislamu zinazojishughulisha na uchinjaji wa
wanyama wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Eid ul Adha kutojihusisha na kuiba
wanyama hao na itakayobaini kufanya wizi huo itachukuliwa hatua kali ikiwemo
kufutiwa kibali cha kufanya kazi hiyo.
Akizungumza katika mkutano na wasimamizi wa
taasisi hizo, maafisa wa Uhamiaji, wafanyabiashara wa nyama, maofisa kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na viongozi kadhaa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) Mkoa wa Singida alisema jambo hilo la wizi wa wanyama wa sadaka
halivumiliki na taasisi itakayo bainika wataishawishi Serikali kuifutia kibali
taasisi hiyo.
"Suala la kuzuia uuzaji wa wanyama kiholela
ni jukumu letu sote hivyo natoa onyo kwa taasisi yoyote inayojishughulisha na
kazi hiyo itakayobainika wanyama wake wameuzwa tutaishawishi Serikali kukifuta
kibali cha kazi hiyo dhidi ya taasisi husika," alisema Nasoro.
Aidha, Sheikh Nasoro alizitaka taasisi hizo
kuchinja wanyama hao kwa kuzingatia haki ya wanyama na taratibu za dini huku
wakitunza mazingira katika maeneo watakapo hifadhiwa wanyama hao kabla na baada
ya kuchinjwa.
Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Singida,
Diana Kisoka akizungumza kwenye mkutano huo aliwaomba wahusika wa taasisi hizo
wageni wao wanaokuja kununua wanyama hao kuwaelekeza kufuata utaratibu wa nchi
wa kuishi badala ya kuwapokea kiholela pasipo kuwa na vibari na baadhi yao
kufikia hatua ya kuoa hadi wake wawili ili kuhalalisha ukaaji wao batili hapa
nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wauza Nyama Mkoa wa
Singida, Omari Palaga alisema uendeleaji wa kuchinja wanyama hao hata baada ya
sherehe hiyo umekuwa ukiwaweka katika hali mbaya ya kiuchumi kufuatia kuwepo
kwa nyama nyingi za bure.
"Sisi wafanya biashara wa nyama soko letu limeharibiwa na wachinjaji wa wanyama wanaoendelea kuchinja hata baada ya sherehe hiyo ya kuchinja huku tukikabiliwa na ulipaji wa kodi mbalimbali za vyumba vya biashara, TRA, usafi, gharama za kuchinja kule machinjioni na nyingine nyingi tunaomba Serikali kuliangalia jambo ili kwa undani zaidi," alisema Palaga.
No comments