' Na Mashaka Kibaya, Tanga
KAMPUNI ya Simba Bingwa kupitia Simba Supply Chain Solution Ltd (SSCS) imeendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake, huku ikijivunia kuwa na vifaa vya kisasa vinavyoiwezesha kuonesha umahiri mkubwa katika kutoa Usuluhishi wa huduma kupitia Bandari ya Tanga.
Meneja wa Kampuni ya Simba Bingwa, Awadhi Massawe ameyasema hayo jana akiwa katika Bandari ya Tanga wakati wakipokea Meli kubwa ya sita yenye jina la Cool Breeze iliyokuwa na shehena ya tani 5000 za Amonium Nitrate kutoka huko nchini Russia.
Massawe amesema, tangu Serikali ilipochukua maamuzi magumu kuwekeza zaidi ya dola Milioni 400 ili kufanya maboresho katika Bandari ya Tanga, mafanikio yameanza kupatikana kwenye ukusanyaji mapato ya Serikali huku Makampuni binafsi nayo yakinufaika.
Alisema kuwa, manufaa mengine yanayopatikana kupitia uwekezaji huo wa Serikali ni fursa za ajira kuongezeka ambapo kila meli inapokuja Simba Supply Chain Solution Ltd inaajiri watu wapatao 150 mpaka 200.
"Maboresho yaliyofanywa na Serikali baada ya kuwekeza zaidi ya dola Milioni 400 yameanza kuleta tija, tunamshukuru Rais Dkt Samia na Viongozi wenzake kwa maamuzi magumu kupanua Bandari ya Tanga, hivi sasa tunanufaika"alisema Massawe.
Massawe amesema kuwa, Simba Supply Chain Solution Ltd inapaswa kuwa chaguo pekee katika utoaji huduma miongoni mwa makampuni kutokana na ukweli kuwa imefanikiwa kuwa na vifaa vya kisasa vya kuhudumia meli kwa haraka na ufanisi.
"Mimi nitoe wito kwa wenye mashirika ya meli,wafanyabiashara Rwanda, DRC, Zambia,Malawi,Uganda na wengine waone fursa kutumia Bandari ya Tanga "alisema Massawe huku akitamba Kampuni yake kuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia.
Massawe alisema, tangu Bandari ya Tanga kukamilika kufanyiwa maboresho imekuwa rahisi kwa meli kubwa kuingia Bandari moja kwa moja huku zikiteremsha bidhaa kwa haraka na hivyo kuepuka gharama zisizo ulazima.
"Sasa kuna uwezekano meli kuingia kwenye ghati na kufunga huku ikianza kupakua mzigo, sio jambo la kawaida sana.Niwaombe wateja wetu waliopo ndani ya Tanzania na nje DRC na kwingine waje Tanga kuna fursa yenye manufaa kwao na hata kwetu kiuchumi"alisema.
Massawe amewasilisha Shukrani zake kwa Mamlaka ya Bandari Makao makuu na Tanga, TRA, watu wa afya, Nemc,Uhamiaji na mamlaka nyingine kwa kuonesha ushirikiano wakati wa utoaji huduma hatua ambayo imekuwa ikirahisisha upatikanaji wa huduma za kibandari.
Aidha Meneja huyo wa Simba Bingwa alisema kwamba, kupitia Simba Terminal wamefanikiwa kununua eneo lenye ukubwa wa ekari 27 Jijini Tanga ili kuweza kulitumia kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya wateja wake.
"Tumepata fursa ya kuwa na ghala moja ndani ya Bandari ya Tanga, hata hivyo katika kukabiliana na ongezeko la shehena kwa vile kuna eneo finyu tumewekeza nje ya Bandari kwa kununua eneo la ekari 27 ya logistic park"alisema.
Kwa uwekezaji huo sasa, Wateja wa Kampuni ya Simba Supply Chain Solution Ltd wataendelea kupata huduma rafiki na wezeshi ambapo Massawe aliendelea kuwahimiza wafanyabiashara kutumia Kampuni yao kupitia Bandari ya Tanga.
Muonekano wa meli hiyo ikiwa Bandari ya Tanga
0 Comments