--------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Na Dotto Mwaibale, Singida
TUME ya Utumishi wa Mahakama imeanza kuchukua hatua zitakazowezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa tume hiyo dhidi ya watumishi wa mahakama wanaokiuka maadili ya utumishi wao.
Hatua hizo zimeanza kwa kutoa mafunzo kwa maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida ambao watawajibilka kuelimisha umma kuhusiana na taratibu wanazotakiwa kufuata kuwasilisha malalamiko yao kwenye tume hiyo.
Naibu Katibu wa Tume hiyo Alesia Mbuya akifungua mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa hao kuhusu majukuu ya tume hiyo hususani kamati za maadili ya Taifa pamoja na za maafisa wa mikoa na wilaya.
Mbuya alisema maafisa tarafa hao ni viongozi muhimu kwenye maeneo yao hivyo wanapaswa kuwajibika ipasavyo kwa wananchi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili wananchi wanaowaongoza waweze kupata haki zao kwa wakati.
Alisema lengo la tume hiyo ni kuhakikisha watumishi wa mahakama wanafuata misingi ya usiri, uadilifu, na ueledi katika kazi na kushirikiana na jamii inayowazunguka.
Mshiriki wa mafunzo hayo Osward Leopold ambaye ni Afisa Tarafa wa Tarfa ya Kisiriri Wilaya ya Iramba alisema wanayo mategemeo makubwa wakiwa kama viongozi kwenye maeneo yao ya kwenda kutoa elimu hiyo walioipata kwa jamii wanayoiongoza.
“Mafunzo haya tunaenda kuyapeleka kwa wananchi wetu tunaowaongoza ili waweze kujua namna ya kupata haki zao pale wanapoona haki zao zimeshindwa kupatikana kutoka kwa wateule wa mahakama,” alisema Leopold.
Kwa upande wake Afisa Tarafa wa Tarafa ya Kilimatinde kutoka Wilaya ya Manyoni, Lyidia Ntitu alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwani watayapeleka kwa wananchi wao wayajue na wakiwa na malalamiko dhidi ya watumishi wa mahakama wajue wapi kwa kuyapeleka.
0 Comments