..............................................
Imeandaliwa na Dotto Mwaibale
(0754-362990)
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa maboresho makubwa ya utoaji wa huduma zake ambayo yameondoa adha ambazo zilikuwa zikiwakabili wananchi.
Chaula ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa shirika hilo ambao uliwahusisha madiwani na viongozi mbalimbali wa halmashauri hiyo wakiwemo wa CCM na baadhi ya wakuu wa taasisi zingine ambao ulifanyika Septemba 6, 2024 kwa lengo la kueleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo pamoja na kuimarisha mahusiano.
Mkurugenzi huyo alisema zamani viongozi mbalimbali walikuwa wakifuatwa na ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wakiwaomba kama wanafahamiana na watumishi wa shirika hilo, wawasaidie kuwaomba ili waingiziwe umeme kwenye nyumba zao lakini hivi sasa jambo hilo limebaki kuwa ni historia kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na shirika hilo.
“Ni kipindi kirefu sasa kimepita sijapata mtu anayeniambia anaangaika Tanesco ili aweze kuingiza umeme na kama nina mtu anayefanya kazi katika shirika hilo nimsaidie,” alisema Chaula.
Chaula alisema kama hakuna mtu anayekwenda kuwaomba viongozi wawasaidie kuingiziwa umeme kwenye nyumba zao kupitia wafanyakazi wa shirika hilo ambao wanawafahamu maana yake ni kwamba Tanesco wamefanya maboresho makubwa wanapaswa kupongezwa kwa kutoa huduma nzuri kwa kadri inavowezekana.
Alisema maboresho hayo yanayofanyika ndani ya Tanesco, mashirika mengine ya kiserikali na yasio ya kiserikali yachukulie ni mfano wa utendaji kazi mzuri wa kuhudumia wanananchi na kutoa ufafanuzi pale panapokuwepo na changamoto kwani mara nyingine shirika linaweza kulaumiwa bure kutokana na watu kutojua kile kinachofanyika na shirika husika.
Chaula akitoa mfano wa maboresho mengine ya Shirika hilo alisema akiwa mkoani Iringa alipiga simu makao makuu ya shirika hilo akitaka msaada baada ya nyumba yake kuwa na changamoto ya umeme lakini haukupita muda alipigiwa simu na Tanesco Mkoa wa Iringa Iringa akiambiwa kuwa wamepigiwa simu kutoka makao makuu hivyo wanaomba aelekeze nyumba yake ilipo ambapo walifika usiku huo huo na kurekebisha kasoro iliyokuwepo.
“Zamani ilikuwa ukipiga simu Tanesco ilikuwa ikichukua siku mbili hadi nne ndipo wafike na iwapo kama ningekuwa Singida pengine watu wangesema nimesaidiwa haraka kwa kuwa ni Mkurugenzi lakini nilipiga simu kama mwananchi wa kawaida, hakika maboresho makubwa yamefanyika ndani ya shirika hilo,” alisisitiza Chaula.
Chaula alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika sekta hiyo kwani vijiji vyote 84 vya Halmashauri ya Wilaya ya Singida vina umeme na sasa wanaelekea kukamilisha kazi hiyo kwenye vitongozi na kwamba kazi hiyo inafanyika kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Alisema Shirika hilo limefanikiwa kufanya maboresho hayo kutokana na mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi wake, Serikali, Wataalamu na wananchi baada ya kupokea maoni yao na kuyafanyia kazi kama wanavyoendelea kukutana na wadau wao nchi nzima na kufanya mikutano hiyo ambayo inaleta tija kwa shirika na Taifa.
Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi Ernest Nyerere alisema kama Tanesco katika kushiriki Mpango wa Taifa wa Nishati waliona ni vema kufanya mkutano huo ili kuwashirikisha wadau wao kuwaelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kama kutakuwa na changamoto zozote ziweze kufanyiwa kazi.
Mhandisi Nyerere ambaye alitoa mada kuhusu usalama alisisitiza jamii kuchukua tahadhari na kutoa taarifa pale wanapoona kuna changamoto yoyote ya miundombinu ya shirika hilo kama nguzo kuanguka au inapotokea itilafu kwenye vifaa vinavyotumia umeme ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo,akizungumzia mkutano huo alisema moja ya lengo lake lingine umelenga kuwaomba madiwani kuwaomba wawekezaji kwenda kuwekeza kwenye mkoa huo.
"Tunawaomba madiwani wahamasisheni wawekezaji kuja kuwekeza katika Mkoa wa Singida tuna umeme wa kutosha kuweza kuwafikia na kuwahudumia kadri watakavyohitaji na upo mwingi," alisema.
Aidha, Mwaipopo aliwaomba watu wanaposafisha mashamba wakati wa misimu ya kilimo kuwa waangalifu wasiunguze miundombinu ya umeme ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kuitengeneza.
Rehema pia alielezea huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.
Kwa upande wake Msimamizi wa miradi wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Anthony Msagwa alisema Wizara ya Nishati kupitia shirika hilo lina mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kuwa na vyanzo mbadala viwili mkoani Singida vya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo na jua.
Moja ya kituo cha kuzalisha umeme kwa njia ya upepo kitajengwa Manispaa ya Singida ambacho kitakuwa na uwezo wa kufua umeme megawati 100 na kile cha kuzalisha umeme kwa njia ya jua kitajengwa Wilaya ya Manyoni ambacho nacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 100.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, Joseph Nyalandu akizungumza kwa niaba ya chama hicho alipongeza Tanesco kwa kufanya mkutano huo na wadau hao ambao aliuelezea kuwa ni muhimu ambapo aliwaomba madiwani hao kwenda kuzungumza mafanikio hayo yaliyofanywa na shirika hilo kupitia Serikali inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
0 Comments