----------------------------------
Na Munir Shemweta, WANMM MLELE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Katavi kuhakikisha eneo la mradi wa maji safi kutoka Majimoto kwenda Usevya linapatiwa hati milki ndani ya wiki mbili.
Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Septema 2024 wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na kiongozi wa mbio za mwenge Godfrey Mnzava katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Mwenge wa uhuru umeanza rasmi mbio zake leo katika mkoa wa Katavi ambapo ulikabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Katavi Bi.Mwanamvua Hozza Mrindoko na mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere.
Amesema, wizara yake imekuwa ikisisitiza mara kwa mara maeneo yote yakiwemo ya umma kumilikishwa kwa hati hivyo ni lazima eneo hilo la mradi wa maji wa Majimoto -Usevya lipatiwe hati ndani ya wiki mbili.
Kauli ya mhe. Pinda inafuatia maelezo kuwa, mradi huo umeshindwa kuendeleza sehemu ya eneo lake kutokana na kutokuwa na hati milki ya eneo hilo jambo lililomshangaza kiongozi wa mbio za Mwenge Godftey Mnzava
" Kiongozi wa mbio za mwenge kufuatia suala hili namuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Katavi kuhakikisha eneo hili linapatiwa hati milki ya ardhi ndani ya wiki mbili" alisema mhe Pinda.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Godfrey Mnzava amesisitiza kuwa, maeneo yote ya umma yamilikishwe kwa hati ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza na kama mwananchi ataamua kutoa eneo lake kwa umma basi taratibu zote za kumilikishwa kwa hati zifanyike.
"Tunasisitiza Maeneo yote ya taasisi yapate milki ambayo ni hati ili kuondoa "confusion' zinazotokea, pale mwamanchi anapoamua kutoa sadaka eneo lake kwa umma na baada ya serikali kulitwaa kinachofuata ni umiliki na lazima utaratibu ufike mwisho wa kupata hati" alisema Mnzava.
Mradi wa maji safi kutoka majimoto kwenda Usevya unatekelezwa kwa fedha za Programu ya Lipa kwa Matokeo ( Payment for Results PloR) kwa mikataba mitano yenye jumla ya ya kiasi cha shilingi 4, 283,137,440.22.
Mradi huo umekusudia kuboresha upatikanaji maji safi na salama katika vijiji vya Usevya, Msadya, Nyambwe, Ikuba na Minyoso kutoka skimu ya Majimogo na wakazi wapatao 34,650 watanufaika na mradi huo.
0 Comments