................................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amevitaka vyama vya siasa nchini kuhamasisha wanachama wao kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili wananchi waweze kuwa na uwanja mpana wa kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo jana kwa vyama vya siasa wakati akitoa takwimu za wananchi waliojiandisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TAMISEMI jijini Dar es Salaam.
Mchengerwa amevishukuru vyama vya siasa kwa kuendeleza ushirikiano, amani na utulivu wakati mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukiendelea.
“Nitoe rai kwa vyama vyote vya siasa kuendelea kuwasihi wanachama wao kudumisha amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kulinda amani, utulivu na ustawi wa nchi yetu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Mchengerwa amevitaka vyombo vya dola kuhakikisha kuwa kuna na amani na utulivu wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea ili wananchi wote waweze kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.
Sanjari na hilo, Mchengerwa amewasisitiza wasimamizi wa uchaguzi na wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi ili mchakato uwe wa huru na wa haki na hatimaye wananchi wote wenye sifa waweze kushiriki.









No comments:
Post a Comment