SHIRIKA LA C.I.P LAKABIDHI MRADI WA HOSTELI SINGIDA, SERIKALI YAOMBWA KUONDOA KODI KWENYE TAULO ZA KIKE - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, October 26, 2024

SHIRIKA LA C.I.P LAKABIDHI MRADI WA HOSTELI SINGIDA, SERIKALI YAOMBWA KUONDOA KODI KWENYE TAULO ZA KIKE

Viongozi mbalimbali wa Kata ya Mwasauya iliyopo Wilaya ya Singida na Maafisa wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida wakielekea kuzindua na kukabidhiwa Bweni la Wasichana wa Shule ya Sekondari ya Mwasauya lililojengwa na shirika hilo kwa ufadhili wa Serikali ya Austria kupitia Shirika la Sister Cities Salzburg –Singida (SCSS) lililoko Salzburg Austria kwa kushirikiana na shirika hilo.

---------------------------------------------------- 

SERIKALI ya Austria kupitia Shirika la Sister Cities Salzburg –Singida (SCSS) lililoko Salzburg Austria kwa kushirikiana na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida limekabidhi mradi wa Hosteli wenye thamani ya Sh. Milioni 160 katika Shule ya Sekondari ya Mwasauya iliyopo Wilaya ya Singida mkoani Singida. 

Mradi huo umetelelezwa na shirika hilo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu katika shule mbalimbali nchini. 

Akizungumza katika hafla ya kuzindua na kukabidhi mradi huo iliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwasauya Oktoba 25, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la C.I.P , Affesso Ogenga alisema ujenzi wa mradi huo wa bweni la wasichana ambalo linauwezo wa kulala wanafunzi 80 kwa wakati mmoja umegharimu Sh. Milioni 160. 

 Ogenga alisema mradi huo umetekelezwa na shirika hilo kwa ufadhili wa wadau waliotajwa hapo juu kwa kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa  Kata ya Mwasauya. 

“ Licha ya kukamilisha ujenzi wa mradi huu kama shirika tumetoa vifaa vyote vinavyotumika humo ndani vitanda vyote 40, makabati ya kuhifadhia nguo na vitu vingine, mapazia na mfumo wa nishati ya umeme wa jua (sola), “alisema Ogenga. 

Alisema shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi katika sekta ya elimu na afya ndani ya Mkoa wa Singida kwa zaidi ya miaka 10 na kutekeleza miradi mbalimbali. 

Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ile waliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano katika Kata ya Ikhanoda na Mwasauya ambapo wamejenda madarasa sita katika shule tatu, ujenzi wa  vyoo vya kisasa vyenye matundu 11 kwenye shule tano ndani ya kata hizo. 

Ogenga aliongeza kuwa mbali ya kazi hizo pia shirika hilo limekuwa likitoa taulo za kike katika shule mbalimbali za msingi katika Kata ya Ikhanoda pamoja na kutoa ufadhili kwa wasichana wanaosoma sekondari na kuwalipia hosteli na wengine wamekuwa wakiwapa baiskeli kwa ajili ya kuwezesha kwenda shuleni. 

Alitaja misaada mingine kuwa ni sare za shule, madaftari, vitabu na vitu vingine vya muhimu  vinavyohusu masomo yao. 

Mkurugenzi huyo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau hao kwa kufadhili miradi hiyo na akatumia nafasi hiyo kuwaaga wanananchi wa kata hizo na kuwaeleza kuwa sasa wanahamia kata kata zingine ambazo hakuzitaja. 

Ogenga alitoa wito kwa wananchi na wanafunzi wa shule hiyo kuitunza miundombinu yote ya miradi iliyotekelezwa kwenye kata hizo ili iweze kudumu na kutumiwa na vizazi vijavyo. 

Kwa upande wake Mratibu wa miradi wa shirika hilo, Violet Shaku, akitoa ujumbe wa shirika aliwaambia wakina mama na akina baba kuwa suala la taulo za kile kwa watoto wao wakiwa shuleni sio jambo la aibu bali wanatakiwa kuwasaidia kuzipata kwani wengi wao wamekuwa na changamoto kubwa hadi kufikia kushindwa kuhudhuria masomo yao kwa siku nne na zaidi wanapokuwa katika hedhi.

Shaku alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali ikiwezekana kuondoa kodi katika bidhaa zote za taulo za kike ili kushusha bei na kila mlengwa aweze kumudu kuzinunua. 

Faudhia Mohammed mwanafunzi wa shule hiyo akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya wenzake alilishukuru shirika hilo kwa kuwajengea bweni hilo ambalo limewaondolea adha waliyokuwa nayo ya kutembea muda mrefu kutoka majumbani kwao kwenda katika shule hiyo. 

Mwanafunzi huyo pia alimshuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha nyingi za kujenga miundombinu ya shule mbalimbali nchini na shule yao ya Mwasauya ikiwa mnufaika wa fedha hizo.

Imeandaliwa na Dotto Mwaibale, Philemon Solomoni (0754-36 2990)

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (katikati( aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo akikata utepea kuashiria uzinduzi rasmi wa bweni hilo.

Uzinduzi wa bweni hilo ukifanyika.
Muonekano wa bweni hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la C.I.P , Affesso Ogenga (katikati) akimuongoza mgeni rasmi, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (kushoto) na Mkuu wa shule hiyo, Adamu Mwakalinga  wakati wa ukaguzi wa bweni hilo kabla ya kuzinduliwa rasmi.
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo Parinemas Mashanjara akizungumza katika hafla hiyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwasauya, Adamu Mwakalinga akizungumza.
Mratibu wa Miradi wa Shirika la C.I.P, Violet Shaku, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la C.I.P , Affesso Ogenga, akizungumzia miradi iliyotekelezwa na shirika hilo.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo. ambayo ilifanyika sanjari na mahafali ya 14 ya wahitimu wa kidato cha Nne wa shule hiyo.
Wahitimu wa kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari ya Mwasauya iliyopo Wilaya ya Singida wakitoa burudani wakati wa mahafali yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la C.I.P , Affesso Ogenga (katikati) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Parinemas Mashanjara (kushoto) na Mratibu wa Miradi wa shirika hilo, Violet Shaku wakati wa hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad