ATCL MPYA CHINI YA MHANDISI PETER ULANGA

Subscribe Us

ATCL MPYA CHINI YA MHANDISI PETER ULANGA

Mhandisi Peter Ulanga Mkurugenzi Mpya Shirika la Ndege Tanzania

...................................

BIDII ya kazi na uzalendo inatajwa kuwa ni moja ya nguzo inayomfanya mtu kusonga mbele katika hatua ya maendeleo yake binafsi na Taifa kwa ujumla hali ambayo tunaiona katika baadhi ya mataifa makubwa kama China ilivyofanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana na watu wake kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii.

Ili kurahisisha utendaji wa kazi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda Taasisi mbalimbali na kuweka wasimamizi lengo likiwa ni kuharakisha maendeleo ya nchi hususani yanayowahusu wananchi katika sekta mbalimbali kama vile elimu, ardhi, maji, umeme, afya. mawasiliano, uchukuzi na nyinginezo.

Wakuu wa taasisi hizo wengi wao wamekuwa wakipatikana kutokana na elimu na taaluma zao, uzoefu wa kazi ambazo wamewahi kuzifanya aidha wakiwa chini ya viongozi wengine au kwa kuteuliwa moja kwa moja na mamlaka za juu.

Leo katika safu hii napenda kumzungumzia Mhandisi Peter Ulanga  Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambaye Rais Samia Suluhu Hassan amemteua jana kushika nafasi hiyo.


 Binafsi namuita mzalendo kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mkurugenzi Mtendaji mwanzilishi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo alifanya maboresho makubwa.

Niseme tu kuwa Mhandisi Ulanga ni kiongozi mzalendo mwenye kuwiwa kuliletea maendeleo Taifa letu na ndio maana hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kumuamini na kumpa nafasi hiyo.

Kila mwenye macho anaweza kuwa shuhuda wa haya ninayosema hivi sasa TTCL ni shirika ambalo lina maboresho makubwa yaliyotokana na uongozi wa Mhandisi Ulanga.

 Kazi hiyo kubwa iliyofanywa na TTCL chini ya Mhandisi Ulanga na timu nzima ya wafanyakazi inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo hasa katika sekta ya mawasiliano hapa nchini, pongezi nyingi ziende kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha shirika hilo kupiga hatua hiyo kubwa ya maboresho.

Kutokana na maboresho hayo makubwa Spika wa Bunge la  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson alilipongeza  shirika hilo kwa kufanya vizuri katika utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na  kufikisha huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. 

Pongezi hizo alizitoa Mei 18,2023 wakati alipotembelea banda la Shirika hilo katika Maonesho yaliyofanyika   viwanja vya Bunge jijini Dodoma. 

Spika Tulia alisema alioneshwa  mambo mengi katika banda la TTCL   lakini suala  la mkongo kufika nyumbani  ni jambo la muhimu   kwani matumizi ya data na teknolojia ni muhimu. 

“Nitume nafasi hii kuwapongeza  TTCL kwa kutuleta huduma hii naamini zitapunguza gharama ya matumizi ya bando ambayo  tumekuwa tunalalamika,” alisema. 

Ebu tuzikumbuke baadhi ya kazi chache kati ya nyingi alizozifanya Mhandisi Peter Ulanga alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Mkurugenzi Mtendaji mwanzilishi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Moja ya kazi iliyofanyika wakati wa uongozi wake ni TTCL na Shirika la Mawasiliano la Burundi (BBS ) yalipotiliana saini hati ya mkataba wa kibiashara wenye lengo la kuongeza huduma kwenye mkongo wa mawasiliano.

Mkataba huo wa Mawasilano wenye thamamani ya  Dola za Kimarekani millioni 3.3 sawa na  Billion  8.3 za  Kitanzania umelenga kuboresha sekta ya mawasiliano sambamba na uboreshwaji wa Matumizi ya Mkongo wa taifa baina ya Nchi ya Tanzania na Burundi na Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) sanjari na Ukanda wa nchi zilizo Kusini mwa Afrika. 

Katika hafla hiyo Mhandisi Ulanga alisema  tukio hilo linakuza mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Burundi na imekuwa ni muhimu kwa mashirikiano ya kiuchumi na kueleza kwamba  wateja wao wameona nguvu kubwa ambayo imekuwa ikiwekezwa katika kuboresha TTCL 

Kazi nyingine aliyoifanya ni Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ikiwemo TTCL zilipoboresha upatikanaji wa huduma za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa jamii ya wafugaji wa Kijiji cha Msomera kilichopo Handeni, Tanga ambao ni wakaazi wapya waliohamia kwa hiyari katika kijiji hicho wakitokea katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Serikali kusaini mkataba wa upanuzi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 23 nchini, wenye urefu wa kilomita 1,520 ambao utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 37 ambao unatekelezwa kwa muda wa miezi sita ni tukio lingine lililoudhuriwa na Mhandisi Ulanga. 

Akizungumza mara baada ya kushuhudia utilianaji saini kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania na Kampuni ya HUAWEI aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye,alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa katika ukuaji wa maendeleo ya Taifa. 

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa kwa wananchi za kiuchumi, kwani kasi ya upatikanaji wa mawasiliano yatachochea maendeleo katika wilaya hizo na Taifa kwa ujumla. 

Mhandisi Ulanga, kuonesha uzalendo wake na kufanya kazi kunakokwenda na muda na kwa ufanisi alisema mkataba huo uliosainiwa unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita tangu kusainiwa kwake na si vinginevyo. 

“Kukamilika kwa mradi huo kutaondoa tatizo lililokuwepo awali la ukosefu wa mawasiliano katika wilaya hizo.”alisema Mhandisi Ulanga.

Hizo ni baadhi ya kazi chache kati ya nyingi zilizotukuka  alizoshiriki kuzifanya Mhandisi Ulanga ambaye anaelezwa kuwa ni kiongozi mwenye uzalendo anaye lipambania taifa kimaendeleo.

Inaelezwa kuwa miaka 20 iliyopita, Mhandisi Ulanga ndiye aliyeandika andiko lililosababisha Watanzania tuanze kununua salio na kukwangua vocha kwa kutumia pesa zetu.

 Kabla ya hapo, tulikuwa tunachajiwa kwa dola za Marekani. Hiyo ilikuwa mwanzoni mwa miaka 2000. 

Imeelezwa kuwa ni Mhandisi Ulanga huyu huyu ndiye aliyekuwa sehemu ya wataalamu wa kimataifa waliokuja na ubunifu wa chaja za simu ambazo sasa zinajulikana kwa jina la type c. 

Ubunifu wake ndiyo umefanya leo watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro wafaidi huduma ya mtandao wa internet na sasa Tanzania ndiyo nchi ambayo mtu anaweza kupata internet akiwa mahali parefu zaidi kwenda juu.

Akiwa katika utumishi wake TTCL kwa nafasi ya Mkurugenzi Rais alimuondoa lakini katika hali ya kushangaza ndani ya siku mbili tangu aondolewe Rais alimrudisha kazini labda baada ya kubaini mambo kadhaa ya utendaji kazi wake mzuri wa kazi.

Ndugu yangu Mhandisi Ulanga pasipo shaka tumeziona jitihada zako unazo zifanya za kulifikisha mbali kiuchumi taifa letu endelea kufanyakazi katika kituo chako kipya cha ATCL kama ulivyoaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bila ya kusahau kuwa hakuna kazi isiyo na changamoto bali endelea kumtegemea Mungu ambaye ndiye muweza wa yote. Kazi Iendelee.

Imeandaliwa na Dotto Mwaibale (0754-362990)

Spika  wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,akimsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga wakati alipotembelea banda la Shirika hilo katika Maonesho yaliyofanyika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma Mei 18,2023. Kushoto ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo.Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga akifafanua  jambo kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye kuhusiana na huduma ya Faiba Mlangoni Kwako ndani ya Banda la TTCL.

Viongozi wa TTCL na Shirika la Mawasiliano la Burundi (BBS ) walipotiliana saini hati ya mkataba wa kibiashara wenye lengo la kuongeza huduma kwenye mkongo wa mawasiliano.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Teknolojia ya Habari ya Kitaifa ya Uganda (National Information Technology Authority of Uganda (NITA-U), Dkt. Hatwib Mugasa walipokuwa wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara mara baada ya kusaini hati hizo za Makubaliano kati ya Shirika la TTCL na Mamlaka ya NITA-U kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB na Mkongo wa Mawasiliano wa Uganda (National Backbone Infrastructures- NBI). 

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter R.Ulanga akizungumza na washiriki wa Kongamano la Wadau wa Mawasiliano na TEHAMA Ndani na Nje ya Tanzania ‘Connect 2 Connect - C2C’ lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga (wa tatu kulia), Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba (wanne kulia) na mwenyekiti wa kijiji cha Msomera, Bw. Martine Oleikai Paraketi katika eneo la ujenzi wa mnara wa mawasiliano wa TTCL wakati wa ziara ya Makatibu Wakuu na Kamati Tendaji kukagua miundombinu na ufikishaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi waliohamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni wakitokea Hifadhi ya Ngorongoro, Julai 7, 2022

 

Post a Comment

0 Comments