Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo akizungumza wakati wa makabidhiano ya mkataba huo.
...........................
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo
ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuingia mkataba na mtoa huduma
kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya
Mkoa wa Mbeya kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja
na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Mpogoro ametoa pongezi hizo leo Novemba 20, 2024
mkoani humo baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa
ugawaji mitungi ya gesi ya uzito wa kilo sita iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa
Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Advera Mwijage.
Mpogoro amesema kuwa mitungi ya gesi
itakayosambazwa mkoani Mbeya itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati
safi na salama.
"Naipongeza REA kwa kuja na mradi huu,
naiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hii muhimu
itakayokuwa mkombozi kwetu, " amesema Mpogoro.
Mwijage amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji.
"Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea,
kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili
kupunguza ukataji wa miti ambapo takribani hekta 400,000 hukatwa kila mwaka,
" ameongeza Mwijage.
Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja
na Wilaya ya Mbeya, Chunya, Kyela, Mbarali na Rungwe
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Advera Mwijage akimkabidhi hati za mkataba wa usambazi wa mitungi ya gesi inayotolewa na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambayo itasambazwa katika wilaya ya Mbeya, Chunya, Kyela, Mbarali na Rungwe.
0 Comments